Na mwandishi wetu
Kipigo cha mechi mbili mfululizo kwenye ligi, kimemuibua Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa akieleza miongoni mwa sababu zinazowaangusha ni kuwa na wachezaji wachache kwa sasa katika kikosi hicho.
Jana Ruvu ilifungwa mabao 2-1 na Geita Gold, ukiwa ni mchezo wao wa nne mfululizo bila ushindi na sasa timu hiyo inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 10 baada ya mechi tisa.
Mkwasa amefafanua kuwa vijana wake wamekuwa wakipambana lakini makosa madogo madogo yamekuwa yakiwaadhibu pia kwa kukosa umakini kwenye eneo lao la hatari kwa kutocheza kwa ustadi mkubwa wa kulinda lango.
“Lakini ni makosa ya kimchezo na jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika kwetu sisi kama benchi na wachezaji na bahati mbaya wengine wapo kwenye ‘kozi’ kwa hiyo tuna kikosi kama cha wachezaji 21 hivi ndiyo ambayo tuko nao.
“Kwa hiyo wanakuwa muda mwingine na uchovu, wanakuwa ni wale wale ambao tunawatumia, sasa nadhani pengine viongozi wanaweza kufanya jambo kuhakikisha wengine wanakuja ili tuwe katika timu nzuri lakini niseme makosa ya kawaida na tutajipanga kuhakikisha tunafanya marekebisho ili turudi kwenye mstari,” alisema Mkwasa.
Soka Wachezaji wachache Ruvu-Mkwasa
Wachezaji wachache Ruvu-Mkwasa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
