Barcelona, Hispania
Klabu ya Barcelona inajiandaa kufungua shauri mahakamani ikiitaka Atletico Madrid iwalipe Euro 40 milioni kwa ajili ya usajili wa Antoine Griezmann.
Mwaka 2021, Griezmann alijiunga na Atletico kwa mkopo wa miaka miwili na klabu hizo kwa sasa zipo katika mgogoro kuhusu kipengele ambacho kinataka mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 na klabu ya Atletico uwe wa kudumu.
Habari za ndani zinadai kwamba Barca wanaamini Griezmann amecheza zaidi ya dakika 45 katika mechi 30 kati ya 37 za msimu uliopita na hiyo kwa mujibu wa Barca maana yake ni kwamba Atletico sasa wanawajibika kumsajili mchezaji huyo na kuwa wa kudumu kwa ada ya Euro 40 milioni.
Kwa upande wao Atletico wanachoamini ni kwamba Griezmann anatakiwa awe amecheza zaidi ya dakika 45 katika asilimia 50 ya mechi anazoweza kupangwa kwa kipindi cha misimu miwili na si msimu mmoja na hivyo kipengele wanachokitumia Barca hakiwezi kufanya kazi.
Griezmann hakuwahi kucheza kwa muda unaozidi saa moja badala yake amekuwa akiingia kipindi cha pili katika mechi za msimu huu, aliingia dakika za 62, 62, 64, 63 na 61 katika mechi tano za timu hiyo.
Inadaiwa kwamba timu ya wanasheria wa Barca imeupitia upya mkataba wao na mchezaji huyo na wanaamini kwamba wapo sahihi lakini tafsiri ya Atletico ipo tofauti na wanachokiamini Barca ingawa msemaji wa Atletico alisema klabu yao haijapokea taarifa yoyote rasmi kutoka Barca au mtu mwingine yeyote kuhusu mpango wa kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria.
Griezmann mwenyewe alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kwamba alimhusu, “Liko nje ya uwezo wangu, mimi nataka kucheza zaidi lakini nitajitoa kwa kila kitu kwa dakika ninazopewa, nina furaha kuwa hapa, kitu pekee ninachotaka ni kujitoa kwa ajili ya klabu hii, kwa ajili ya mashabiki na kocha Diego Simeone.”
Naye kocha wa Barca, Xavi alipoulizwa alisema, “Hilo halinihusu, ni suala la linalohusu klabu mbili, si jambo ambalo nimehusishwa, klabu mbili zinatakiwa kuzungumza, lakini si jambo la kuzua mjadala, tunafikiri ni mchezaji wa Atletico Madrid.”
Kocha Simeone ana imani na mchezaji huyo kwamba anaweza kuwa na mchango mkubwa lakini hofu ya Atletico ni kutoa Euro milioni 40 kwa mchezaji ambaye kabla ya mwisho wa msimu huu atakuwa amefikisha umri wa miaka 32 wakati Barca haina nia ya kumchukua mchezaji huyo hasa kwa kuwa mshahara wake unazidi Euro milioni 20 na hivyo kuwaingiza katika tatizo la matumizi ya fedha ambayo yanakwenda kinyume na taratibu.
Griezmann alijiunga na Barca mwaka 2019 kwa ada inayotajwa kufikia Euro 100 milioni akitokea Atletico, ameifungia Barca mabao 35 katika misimu yake miwili na timu hiyo kabla ya kurudi Atletico, timu ambayo alijiunga nayo mara ya kwanza mwaka 2014 akitokea Real Sociedad.
Kimataifa Barca, Atletico kortini, kisa? Griezmann
Barca, Atletico kortini, kisa? Griezmann
Related posts
Read also