Na mwandishi wetu
Bao pekee la kujifunga la Yahya Zayd limeiwezesha Simba kubeba Kombe la Shirikisho CRDB mbele ya Azam FC katika mechi ya fainali iliyochezwa Jumamosi Julai 4, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Beki huyo tegemeo wa Azam alijifunga bao hilo kwa bahati mbaya na kuineemesha Simba katika dakika ya 62 alipokuwa akijaribu kuokoa krosi iliyopigwa na kiungo wa Simba, Elly Mpanzu.
Juhudi za Azam kusaka bao la kusawazisha zilipata pigo dakika chache baadaye walipojikuta wakibaki wachezaji 10 uwanjani baada ya kiungo wao Feisal Salum au Fei Toto kulimwa kadi nyekundu.
Fei, mmoja wa wachezaji muhimu wa Azam alipewa kadi hiyo baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Simba, Libasse Gueye na mwamuzi kumpa kadi hiyo hapo hapo.
Kutolewa kwa Fei kuliwaweka pagumu wachezaji wa Azam ambapo juhudi zao za kutafuta bao la kusawazisha zilizidi kuwa ngumu na haikushangaza dakika 90 kumalizika Simba wakitowa vifua mbele na bao hilo pekee.
Simba wamelibeba taji hilo lililokuwa likishikiliwa na mahasimu wao Yanga ambao waliweka rekodi kwa kulibeba kwa misimu minne iliyopita.
Katika msimu huu wa 2025-26 Yanga wameishia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB ambapo walishindwa kutamba mbele ya Azam baada ya kuchapwa mabao 3-2.
Kimataifa Simba yatwaa taji la Shirikisho CRDB
Simba yatwaa taji la Shirikisho CRDB
Read also
