Tirana, Albania
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ghana, Raphael Dwamena, 28, amefariki dunia uwanjani akiwa kwenye mechi ya ligi ya soka nchini Albania.
Dwamena (pichani) ambaye ameichezea timu ya Taifa ya Ghana mara tisa na kuifungia mabao mawili, alikutwa na umauti jana Jumamosi dakika ya 23 katika mechi ambayo timu yake ya Egnatia ilikuwa ikiumana na Partinzani.
“Licha ya juhudi za madaktari wataalam kuwahi na kumpa huduma kwa bahati mbaya alifariki dunia,” ilieleza taarifa ya Chama cha Soka Albania (AFL).
Dwamena alikuwa ndiye mfungaji anayeongoza katika Ligi ya Albania msimu huu akiwa amefunga mabao tisa, kifo chake kimesababisha kusimama kwa ligi ya Albania kwa kipindi cha wiki nzima.
AFL kama ilivyo kwa Chama cha Soka Ghana (GFA) kwa pamoja wametoa taarifa za masikitiko yao juu ya kifo cha mchezaji huyo na kuipa pole familia ya mchezaji huyo katika kipindi hiki kigumu.
Rais wa GFA, Edwin Simeon Okraku alisema kwamba Dwamena alikuwa mchezaji aliyeiwakilisha vizuri nchi yake pale alipohitajika na kuonesha uwezo wake.
Mwaka 2017 mpango wa Dwamena kujiunga na klabu ya Brighton ya England kwa ada ya Pauni 14 milioni ulikwama baada ya vipimo vya afya kuonesha kuwa mchezaji huyo hakuwa sawa.
Hata hivyo baadaye alizichezea timu za Levante ya Hispania katika La Liga na pia aliwahi kucheza kwa mkopo katika klabu ya Real Zaragoza pia ya Hispania.
Mwaka 2021 alianguka uwanjani kwenye mechi ya kikombe nchini Austria wakati timu aliyokuwa akiichezea ya Blau-Weiss Linz ikiumana na Hartberg ingawa tukio hilo halikumfanya aachane na soka na baadaye kukawa na habari kwamba alifanyiwa operesheni ya moyo.
Mwaka 2019 wakati akiichezea Real Zaragoza zilikuwapo habari kwamba Dwamena alikuwa na mpango wa kustaafu soka kutokana na hofu ya kupata matatizo makubwa ya moyo.
Habari hizo zilikuja baada ya mchezaji huyo kwenda Barcelona, Hispania na kukutana na madaktari waliobebea kwenye magonjwa ya moyo ingawa bado aliendelea kucheza soka hadi umauti ulipomkuta jana Jumamosi.
Kimataifa Mchezaji Ghana afariki uwanjani Albania
Mchezaji Ghana afariki uwanjani Albania
Related posts
Read also