Paris, Ufaransa
Wakala wa Karim Benzema amesema mshambuliaji huyo angeweza kuwa tayari kucheza mechi ya hatua ya 16 (mtoano) ya fainali za Kombe la Dunia lakini kocha Didier Deschamps na jopo la madaktari wa timu hiyo waliamua kumuondoa kikosini.
Novemba 19, Benzema alipatwa na tatizo la misuli ya paja akiwa mazoezini siku tatu kabla ya Ufaransa kucheza mechi yake ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia na mabosi wa Shirikisho la Soka Ufaransa wakasema atahitaji wiki tatu hadi kupona.
Kocha Deschamps baada ya kufanya mashauriano na daktari wa timu ya Ufaransa, Franck Le Gall waliamua Benzema aondolewe kwenye kikosi cha timu ya Taifa lakini alienda kufanya mazoezi na Real Madrid na baaadaye akatangaza kustaafu kuichezea Ufaransa.
“Nimewasiliana na wataalam watatu, wamethibitisha Benzema angeweza kuwa sawa na kucheza katika mechi za hatua ya 16 walau kuwa kwenye benchi,” alisema wakala huyo, Karim Djaziri kupitia akaunti yake ya Twitter akionyesha picha ya video ya mchezaji huyo akiwa katika hospitali moja ya Qatar na kuhoji ni kwa nini walimtaka aondoke haraka.
“Wiki moja baada ya kuondoka kwenye timu ya Ufaransa, Benzema alianza kukimbia kwa mara nyingine, baada ya siku nne za mazoezi akacheza kwa dakika 30 mechi ya kirafiki ya Real Madrid… endeleeni kudanganya, ukweli unakuja,” aliongeza Djaziri.
Ufaransa ambao walitwaa taji la dunia mwaka 2018, katika fainali za Qatar 2022 walifikia hatua ya fainali kabla ya kushindwa kutamba mbele ya Argentina walioibuka mabingwa wapya wa dunia kwa mikwaju ya penalti 4-2.
Benzema anaamini kuwa Deschamps hakumthamini na ndio maana hakuwa tayari kuendelea kuwa naye katika kikosi hicho hadi hatua ya mtoano (16) ingawa kocha huyo naye aliamini majeraha ya mchezaji huyo yalikuwa makubwa na isingekuwa sahihi kuendelea kuwa naye kikosini.
