London, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag hana wasiwasi na kipa wake David de Gea licha ya kipa huyo kufanya kosa lililoipa West Ham bao jana Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
De Gea (pichani) alifanya kosa ambalo Said Benrahma alilitumia na kuipa West Ham ushindi wa bao 1-0, matokeo ambayo yameifanya Man United ijikwaze katika mbio za kuwania ‘top four’ ya EPL.
Na ingawa Man United inashika nafasi ya nne kushindwa kupata pointi mbele ya West Ham kunaifanya ishindwe kuongeza tofauti ya pointi kati yake na Liverpool inayoshika nafasi ya tano ikiwa na pointi 62 wakati Man United ina pointi 63 ingawa Man United imecheza mechi 34 na Liverpool 35. Man United pia ingeweza kupanda hadi nafasi ya tatu na kuipiku Newcastle iliyopoteza mechi yake na Arsenal.
Siku kadhaa zilizopita kumekuwa na mjadala kuhusu majaliwa ya De Gea ndani ya kikosi cha Man United na nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo lakini Ten Hag ameendelea kusisitiza kuwa bado ana imani na kipa huyo raia wa Hispania.
“Ni kipa mwenye ‘clean sheets’ nyingi katika ligi kuu kwa hiyo tusingeweza kuwa hapa tulipo bila ya yeye,” alisema Ten Hag katika mkutano na waandishi wa habari.
“Kwa hiyo ana imani yangu kwa asilimia zote, sina wasiwasi naye, makosa yanatokea lakini katika timu ni lazima mkabiliane nayo, ni lazima muonyeshe ubora, utulivu na kujirudi na hicho ndicho ambacho hii timu itakifanya,” aliongeza Ten Hag.
Mkataba wa De Gea na Man United unafikia ukomo majira ya kiangazi baadaye mwaka huu ingawa mazungumzo ya kumuongezea mkataba yanaendelea.
Katika siku za karibuni Man United imekuwa ikihusishwa na mipango ya kusajili makipa kadhaa lakini akimzungumzia De Gea, Ten Hag alisema kwamba kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 ataendelea kuwa katika klabu hiyo msimu ujao.