Na mwandishi wetu
Kiungo Stephan Aziz Ki amedhihirisha thamani yake katika kikosi cha Yanga baada ya kufunga mabao matatu (hat trick) wakati timu hiyo ikiinyuka Kagera Sugar mabao 5-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Ushindi huo wa kupendeza umepatikana Jumanne hii kwenye dimba la Azam Complex wakati ambao Yanga inajiandaa kuwakabili mahasimu wao Simba Jumapili ijayo katika mechi nyingine ya ligi hiyo.
Nyota ya Aziz Ki katika mechi hiyo ilianza kung’ara dakika ya 41 alipoifungia Yanga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti kabla ya kuongeza la pili dakika tatu baadaye akifumua shuti kali nje kidogo ya eneo la 18.
Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, Fiston Mayele aliipatia Yanga bao la tatu baada ya kuwazidi ujanja mabeki na kuchomoka kwa kasi kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni.
Mayele ambaye baadaye alitolewa na nafasi yake kuingia Clement Mzize, kwa bao hilo anakuwa amefikisha mabao 16 kwenye ligi akiwa ndiye kinara wa mabao wa ligi hiyo hadi sasa.
Yanga iliandika bao la nne katika dakika ya 84 likifungwa na winga matata wa timu hiyo, Benard Morisson ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Farid Mussa.
Aziz Ki alikamilisha karamu ya mabao ya Yanga katika dakika ya 90 alipofunga bao lake la tatu katika mechi hiyo na la tano kwa Yanga, bao hilo pia likipatikana kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi huo Yanga inazidi kujiimarisha kileleni ikiwa imefikisha pointi 68 na kuzidi kuwakimbia mahasimu wake Simba ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 60.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, mambo yaliendelea kuwa magumu kwa KMC baada ya kuchapwa na Geita Gold mabao 2-0, matokeo ambayo yanafifisha juhudi za timu hiyo kujinasua na janga la kushuka daraja.
Soka Aziz Ki aipendezesha Yanga
Aziz Ki aipendezesha Yanga
Read also