Milan, Italia
Kiungo wa Juventus, Paul Pogba amebainika kutumia dawa za kusisimua misuli na huenda akajikuta akifungiwa kucheza soka kwa miaka minne.
Agosti 20 katika mechi ya Serie A kati ya Juventus na Udinese, Pogba ambaye alikuwa katika benchi la Juventus, alichukulwa vipimo na Kamisheni ya Kuzuia Dawa za Kusisimua Misuli ya Italia (Nado).
Taarifa ya Nado iliyopatikana jana Jumatatu ilieleza kuwa baada ya kipimo hicho Pogba anasubiri vipimo vingine vya ziada kabla ya kushitakiwa na huenda akafungiwa kucheza soka miaka minne.
Kwa sasa Nado wameamua kumsimamisha Pogba wakati akisubiri taratibu nyingine zikiendelea kabla ya kuchukuliwa kwa uamuzi wa mwisho ambao pia utatoa ufafanuzi wa tukio zima.
Klabu ya Juventus ilitoa taarifa kuhusu kilichotokea kwa ufupi pamoja na kusimamishwa kwa mchezaji huyo na kuahidi kuweka wazi hatua inayofuata katika sakata hilo hapo baadaye.
“Tunasubiri matokeo ya vipimo vingine na kwa sasa hatuwezi kusema lolote, jambo linalotia shaka ni kwamba Paul Pogba katu hakuwahi kuwa na dhamira ya kuvunja sheria,” alisema Rafaela Pimenta ambaye ni wakala wa Pogba.
Kilichomkuta Pogba ni pigo jingine kwa mchezaji huyo ambaye tangu atue Juventus akitokea Man United zaidi ya mwaka mmoja uliopita amekuwa akiandamwa na majeraha hadi kushindwa kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar, Novemba na Desemba mwaka jana.
Kabla ya kadhia ya madawa ya kusisimua misuli kuibuka, inadaiwa Pogba alinukuliwa akisema kwamba anafikiria kustaafu soka.
Baada ya kuwa na wakati mgumu msimu uliopita, ilitarajiwa Pogba angeiwakilisha vizuri Juventus msimu huu, timu ambayo msimu uliopita iliandamwa na kashfa ya upangaji matokeo lakini hadi sasa mchezaji huyo amecheza mechi mbili tu tena akitokea benchi.
Kimataifa Pogba kufungiwa miaka minne
Pogba kufungiwa miaka minne
Read also