Na mwandishi wetu
Vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga wameendelea kudhihirisha umahiri wao katika ligi hiyo kwa kuichapa Mbeya City mabao 6-0 katika mechi iliyopigwa Alhamisi Machi 16, 2026 kwenye dimba la KMC, Mwenge Dar es Salaam.
Yanga ilianza kuonesha makali yake katika dakika ya saba ya mchezo huo kwa bao la Prince Dube aliyeutumia vyema mpira wa kona uliopigwa na Pacome Zouzoua.
Wakati Mbeya City wakianza kupambana kutaka kusawazisha bao hilo, dakika tatu baadaye walikatishwa tamaa kwa kufungwa bao la pili lililofungwa na Pacome.
Hali ikazidi kuwa ngumu kwa timu hiyo kutoka Mbeya baada ya kuchapwa bao la tatu mfungaji akiwa Maxi Nzengeli kabla ya timu hiyo kuokota tena mpira kwenye nyavu zao dakika ya 44 kwa bao la Pacome.
Katika dakika za nyongeza kabla ya timu kwenda mapumziko, Mohamed Hussein Zimbwe Jr aliipatia Yanga bao la tano baada ya kuinasa pasi ya Alan Okelo na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko Yanga wakiwa mbele kwa mabao 5-0.
Bao la sita lililohitimisha karamu ya mabao ya Yanga lilijazwa wavuni kwa mara nyingine na Prince Dube katika dakika ya 82
Ushindi huo unazidi kuiimarisha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi wakati kwa Mbeya City hali inazidi kuwa mbaya ambapo katika mechi zake 19, timu hiyo imekusanya pointi 17 tu ikizidi kujiweka katika hatari ya kushuka daraja.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Mashujaa na Singida Black Stars ziligawana pointi moja moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1, mabao ya washindi yakifungwa na Elvis Rupia kwa Singida BS na Mgandila Shaaban kwa Mashujaa.
Soka Yanga yaisulubu Mbeya City 6-0
Yanga yaisulubu Mbeya City 6-0
Read also
