Lens, Ufaransa
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri kuumia kwa Bukayo Saka (pichani) ni jambo lililoleta hofu ingawa hajutii kumpanga katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana Jumanne dhidi ya Lens, mechi ambayo Arsenal ililala kwa mabao 2-1.
Saka aliumia katika mechi mbili za Ligi Kuu England lakini katika hali ambayo haikutarajiwa alipangwa katika mechi ya jana kwenye dimba la Bollaert-Delelis na kucheza kwa dakika 34 kabla ya kutolewa akiwa na maumivu ya misuli.
Mchezaji huyo ndiye aliyepika bao la kwanza la Arsenal lililofungwa na Gabriel Jesus lakini Lens walisawazisha kupitia Adrien Thomasson kabla ya kuongeza la pili lililofungwa na Elye Wahi na kuwa kipigo cha kwanza kwa Arsenal tangu kuanza kwa msimu huu.
Saka ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England anatarajia kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa majeraha aliyonayo lakini ana uwezekano mdogo wa kucheza mechi ya Jumapili ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Man City.
“Alijaribu kupiga mpira kwa nyuma katika kipindi cha kwanza na akajikuta katika hali tofuati, ni tatizo la misuli, alijisikia vibaya na tukalazimika kumtoa nje,” alisema Arteta.
“Hatuna tunachojua zaidi ya hilo lakini ni wazi lilikuwa tatizo kubwa la kumzuia kuendelea kucheza na hilo ni dhahiri kwamba linatupa hofu, sina ninachojua kuhusu mechi ijayo, sijui,” alisema Arteta.
Alipoulizwa kama anajuta kumpanga Saka katika mechi hiyo, Arteta alisema, “hapana, ni maumivu aliyoyapata siku nyingine na akawa vizuri kabisa, ni tukio la kupiga mpira kwa nyuma ambalo linaweza kusababisha aina hii ya maumivu, ngoja tujue ukubwa wa tatizo.”
“Maumivu yaliyopita yalikuwa ya kawaida, hakukosa mechi nyingi, tulimpumzisha katika mechi na Brentford, hivyo ndivyo ilivyokuwa,” alisema Arteta.
