London, England
Makocha Jurgen Klopp wa Liverpool na Pep Guardiola wa Manchester City, kila mmoja ametoa kauli inayoashiria kuihofia timu ya mwenzake wakati timu zao zikijiandaa kuumana Jumapili hii katika mechi inayotarajiwa kuwa ngumu.
Pep ameanza kwa kuwatahadharisha wachezaji wake kuwa hawatakiwi kuwa ‘laini’ katika mechi hiyo huku akisisitiza kwamba Liverpool licha ya kuanza vibaya msimu huu, anaamini bado ni wapinzani wao wakuu katika mbio za kuliwania taji la Ligi Kuu England (EPL).
Kocha huyo anaamini kuwa ni mapema mno kuitoa Liverpool katika mbio za kulisaka taji hilo hasa kwa mafanikio ambayo timu hiyo imeyapata msimu uliopita ikiwa karibu kubeba taji la EPL na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa upande wake Klopp alimsifu mshambuliaji wa City, Erling Haaland akisema kwa sasa ndiye mshambuliaji bora duniani hivyo ni lazima watafute mbinu za kumdhibiti japo alitahadharisha kwamba kumdhibiti Haaland pekee kunaweza kuwapa nafasi wachezaji wengine wa City kuwaadhibu.
Kocha huyo pia ameisifia City akisema kwa sasa ndiyo timu bora duniani ingawa atajaribu kuidhibiti katika mechi ya Jumapili akibebwa na nguvu ya mashabiki wao kwenye dimba la Anfield.
Ni vigumu kujua kama makocha hao wanamaanisha wanachokisema au ni mbinu za mchezo kutokana na ugumu wa mechi hiyo lakini kimsingi kauli zote zinabeba ukweli japo ni kama vile kila mmoja anamtega mwenzake.
Hakuna asiyejua makali ya Haaland hasa kwenye EPL, namba zake zinathibitisha kila kitu, ndiye kinara wa mabao wa ligi hiyo akiwa na mabao 15 katika mechi tisa na mabao 20 katika michuano yote hadi sasa, rekodi ambazo ni uthibitisho tosha wa mchezaji mahiri anayeweza kuiadhibu timu yoyote pinzani.
Kauli ya Klopp hata hivyo kudai kwamba Haaland ni mshambuliaji bora duniani inaweza kuwa mbinu ya kimchezo ya kumvimbisha kichwa mshambuliaji huyo au imekuja mapema mno kwani ligi bado mbichi.
Pep naye kitendo chake cha kuitaja Liverpool kuwa bado ni mshindani wao mkuu katika mbio za kuliwania taji hilo kwa sasa ina kila uhalali kutokana na mambo ambayo timu hiyo imeanza kuyafanya hasa Ulaya baada ya kuibugiza Rangers mabao 7-1 katika Ligi ya Mabingwa huku Mohames Salah akifunga mabao matatu peke yake kati ya hayo.
Makali ambayo ameanza kuyaonesha Salah, mshambuliaji bora wa timu hiyo msimu uliopita yanatosha kumtia hofu Pep kuamini kwamba huenda timu inayofuata baada ya Rangers ni City hasa kwa mabadiliko aliyofanya Klopp katika mechi na Rangers kwa kumpanga Salah katikati, mabadiliko yaliyozaa matunda au Liverpool imeanza kurudi katika ubora wake na si tena timu ya kuibeza.
Upande wa pili hata hivyo namba zinaonesha jinsi Liverpool inavyojikongoja katika EPL ikiwa nafasi ya 10, imezidiwa kwa pointi 13 na Man City inayoshika nafasi ya pili, hivyo Pep anapoitaja timu hiyo kuwa ni mshindani wao mkuu katika ligi hiyo kidogo kauli hiyo inatakiwa kutiliwa shaka kwamba ina ukweli au ndio mbinu zenyewe za kimchezo.
Kwa hiyo mbali na makocha hao kutoa kauli zinazoonesha kuogopana lakini kwa upande wa pili kauli hizo ni kama za kutegana, kila mmoja akimtega mwenzake kwa kauli za kumpamba. Yote kwa yote dakika 90 zitatoa jibu sahihi.
Kimataifa Pep, Klopp waanza kuogopana
Pep, Klopp waanza kuogopana
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
