Na mwandish wetu
Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga kesho Jumamosi watakuwa viwanja viwili tofauti katika mechi zao za pili za hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Yanga itakuwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikitafuta ushindi wa kwanza dhidi ya Al Ahly baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya CR Belouizdad, Uwanja wa Julai 5, Algiers.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema jana kuwa wamejiandaa vizuri wakifahamu wanakutana na timu bora zaidi Afrika na wako tayari kuchuana nao akiwaamini mno vijana wake katika kusaka ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi wa kombe hilo.
“Tangu mwanzo wa msimu tumefanya kazi kubwa kufika hapa, moja ya malengo yetu kuwa hapa kwamba mashabiki, hata wengine wana matarajio nasi makubwa. Hii ni furaha kwetu kucheza na kupambana na timu kubwa yenye mafanikio Afrika na tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi.
“Lakini ninajiamini, nina imani kubwa na kundi la wachezaji nilionao kwamba wanaweza kusimamia hali ya ushindani huo na kupata matokeo mazuri na kama nilivyosema tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kesho, pointi kubwa ni kutorudia makosa yaliyotugharimu kwenye mechi ya kwanza,” alisema Gamondi.
Kabla ya mchezo huo, timu hizo katika mechi 10 za jumla walizowahi kukutana, Yanga imeshinda mechi moja, Al Ahly wameshinda mara sita na sare tatu.
Timu hizo zilikutana mara ya mwisho kwenye mchezo wa raundi ya kwanza kuingia makundi ya michuano hiyo mwaka 2016, mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya bao 1-1 kabla ya Al Ahly kupata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani kwao.
Al Ahly inaingia uwanjani ikiwa kinara wa Kundi D kwa pointi tatu baada ya kuifumua Medeama kwa mabao 3-0, nafasi ya pili ni Belouizdad, inafuata Medeama isiyo na pointi sawa na Yanga iliyo mkiani mwa kundi hilo.
Upande wa Simba ambayo iliondoka nchini alfajiri na kufika leo asubuhi nchini Botswana, wameeleza wako tayari kuwakabili Jwaneng wakifahamu ni mechi ngumu lakini uwepo wa kocha wao mpya, Abdelhak Benchika unawapa morali ya ushindi.
Kama ilivyo Yanga, Simba nayo inatafuta ushindi wa kwanza msimu huu kwenye makundi baada ya mechi yao iliyopita dhidi ya ASEC Mimosas iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Pia mechi hiyo ni kama nafasi ya Simba kulipa kisasi baada ya Jwaneng kuwakwamisha Wekundu hao kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2021-22 kwa matokeo ya Simba kushinda ugenini mabao 2-0 kisha kufungwa kwa Mkapa mabao 3-1 na Jwaneng kusonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini.
Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Hii Jwaneng ya sasa si ile tuliyoifunga kwao wakati ule, wamebadilika na hata kocha wao amekaa nao muda mrefu hivyo wana muunganiko mzuri zaidi na ni timu ngumu.
“Kwa kufahamu hilo tunakwenda kwa umakini mkubwa ila yote kwa yote tunahitaji ushindi na tuaamini tutaupata, mabadiliko ya wiki moja hii inatupa kujiamini, ujio wa Benchikha unatupa kujiamini maana uzoefu alionao katika michuano hii unatosha kutupa kitu katika ile mipango ya muda mfupi ya makocha,” alisema Ally.
Timu hiyo ambayo imetua Botswana na kikosi cha wachezaji 20, inatarajia kukipiga kwenye Uwanja wa Obed Chilume, Francistown kuanzia saa 10 jioni.
Mpaka sasa katika msimamo wa Kundi B, Jwaneng inaongoza kwa pointi tatu baada ya kuifunga Wydad AC bao 1-0, ASEC ni ya pili ikiwa na pointi moja sawa na Simba huku Wydad ikiburuza mkia bila ya pointi.