Na mwandishi wetu
Siku chache baada ya beki wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo, amesema yupo tayari kupambania namba kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.
Ninja ambaye ametoka kwenye majeraha ya goti yaliyomuweka nje kwa msimu mzima, pia ameshukuru kupewa nafasi nyingine ya kuonesha alichonacho akiwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa atafanya vizuri safari hii.
“Nashukuru kupata nafasi ya kuongeza mwaka tena kwenye timu ambayo ni nafasi pekee maana kwa msimu uliopita nilikuwa na majeraha yaliyokuwa yananifanya nikae nje kwa msimu mzima lakini sasa hivi niko sawa naamini kwa uwezo wa Mungu nitafanya vizuri.
“Hii ni nafasi nyingine ambayo nikipata nafasi nitaweza kuitumia vizuri na kuwarejeshea kile nilichonacho, japokuwa kocha mwenyewe ndiyo huwa ana mapendekezo yake ila kwa upande wangu nimejipanga vizuri nitakapopata nafasi nitaitumia vya kutosha,” alisema Ninja.
Ninja ambaye alijiunga Yanga misimu miwili iliyopita akitokea MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech anatarajia kukutana na changamoto ya namba kutoka kwa mabeki Dickson Job na Abdallah Mwamnyeto wanaotumika katika nafasi hizo.
Kiungo mkabaji, Yanick Bangala pia anaweza kuwa kikwazo kwa Ninja kutokana na umahiri wake wa kutumika katika nafasi hiyo inapotokea anakosekana mmoja kati ya Job na Mwamnyeto. Beki mwingine Ibrahim Bacca naye anatajwa kuwa changamoto kwa Ninja.
Soka Ninja kupigania namba Yanga
Ninja kupigania namba Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
