Na mwandishi wetu
Simba imewaita wachezaji wake mastaa waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa kuripoti keshokutwa kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi zao za Ligi Kuu Bara zilizosalia.
Wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa ni Meddie Kagere wa Rwanda, Rally Bwalya (Zambia) wengine ni Aishi Manula, Kennedy Juma, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin na Kibu Denis waliokuwa Taifa Stars.
Pamoja na hayo, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa mbali na wachezaji hao pia wanatarajia kuwasili kwa kiungo wao, Clatous Chama aliyekwenda kwao Zambia kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo cha mkewe pamoja na kutibiwa goti lake.
“Baada ya kukamilika kwa ratiba ya mechi za Fifa tulitoa mapumziko ya siku mbili na tarehe 11 (keshokutwa) wachezaji wote waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa wanatarajia kuripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi za ligi tulizonazo.
“Hiyo pia inajumuisha kurejea kwa Chama ambaye aliondoka kwa sababu za kumbukumbu ya kifo cha mkewe na kuunganisha pia kupatiwa matibabu ya goti lake, vipimo alivyofanya Bugando (Mwanza) ilionekana bado anahitaji matibabu kidogo kwa hiyo akirejea tutamuangalia zaidi,” alisema Ally.
Simba inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 51 dhidi ya Yanga iliyo kileleni kwa pointi 64, inatarajia kukamilisha mechi zake tano zilizosalia kwa kuanza kuivaa Mbeya City dimba la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Ally amesisitiza kuwa ushindi kwao ni muhimu kila mechi.
“Pamoja na yote lakini wachezaji wanatambua kwamba tunahitaji matokeo na tunahitaji ushindi katika mechi zote zilizobaki, hilo ni deni kwa wachezaji kuhakikisha kwamba tunamaliza vizuri, hivyo maandalizi yataendelea kwa kiwango cha juu kuhakikisha tunapata ushindi mechi zote,” alisema Ally.
Soka Mastaa Simba waitwa kambini
Mastaa Simba waitwa kambini
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
