Na mwandishi wetu
Simba imeiengua Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Tabora United mabao 3-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa leo Jumapili, Februari 2, 2025.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 43 na kuizidi Yanga kwa tofauti ya pointi moja, baada ya Yanga kushika nafasi hiyo kwa takriban saa 24.
Simba ilianza kuzitikisa nyavu za Tabora katika dakika ya 12 kwa bao la Leonel Ateba aliyefumua shuti kali lililomshinda kipa wa Tabora, Jean Amonome.
Wenyeji Tabora wakiwa kwenye dimba lao la Ali Hassan Mwinyi walipambana kusawazisha bao hilo kabla ya kuvunjwa nguvu dakika ya 32 baada ya Simba kuandika bao la pili lililofungwa tena na Ateba.
Ateba alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Kefa Kayombo baada ya Faria Odongo kumchezea rafu Elly Mpanzu, rafu ambayo pia ilimfanya Odongo apewe kadi ya njano.
Juhudi za Ateba zilizalisha bao la tatu kwa Simba ambalo lilifungwa na beki Shomari Kapombe katika dakika ya 66.
Kwa matokeo hayo Tabora inabaki nafasi ya tano ikiwa na pointi 25, imetanguliwa na Singida Big inayoshika nafasi ya nne na pointi zake 33 wakati Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36.
Kimataifa Simba yaiengua Yanga kileleni
Simba yaiengua Yanga kileleni
Read also
