Na mwandishi wetu
Makocha wapya wa Azam FC, Dani Cadena na Mikel Guillen wametua nchini usiku wa kuamkia leo wakiwa tayari kwa ajili ya kazi mpya ya kukinoa kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2022-23.
Cadena ambaye ni kocha wa makipa na Guillen ambaye ni kocha wa viungo wote wakiwa ni raia wa Hispania wanaungana na kocha mpya wa washambuliaji, Kali Ongala na kocha mkuu, Abdihamid Moallin kwa ajili ya kikosi kazi cha msimu ujao.
Guillen anasifika kwa uwezo mkubwa wa kuwaweka fiti wachezaji katika timu za Aris Limassol ya Cyprus, Belanguru ya India na Dinamo Bucurest ya Romania alikowahi kufundisha wakati Cadena mwenye alimu ya juu ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) akiwa pia amewahi kufanya kazi Sevilla na Real Betis za Ligi Kuu ya Uhispania.
Kulingana na wasifu wa makocha hao, Azam inaamini itakwenda kuleta changamoto kubwa kwenye michuano watakayoshiriki ya Ligi Kuu ya NBC Bara, Kombe la FA pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ujio wa makocha hao ambao wametua wakitokea kwao Hispania, umekamilisha jopo la kikosi kinachotarajiwa kwenda Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Azam ambayo msimu uliopita imemaliza kwenye nafasi ya tatu, inaanza rasmi kesho mazoezi na maandalizi hayo kabla ya kuondoka nchini kuelekea Misri Ijumaa hii wakitarajiwa kurejea nchini Agosti 12, mwaka huu.
Soka Makocha wapya Azam watua Dar
Makocha wapya Azam watua Dar
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
