Na mwandishi wetu
Baada ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Mapinduzi, kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema licha ya kutaka ubingwa pia anaitumia michuano hiyo kutoa nafasi kwa wachezaji wote kikosini kuimarisha viwango vyao.
Yanga imetinga robo fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jamus ya Sudan Kusini jana usiku Jumanne, mtanange uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja, Zanzibar.
Mara ya mwisho kwa Yanga kutwaa Kombe la Mapinduzi ilikuwa mwaka 2021 ilipoibuika na ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Simba.
Gamondi raia wa Argentina alisema ulikuwa mchezo mgumu kutokana na wapinzani wao kucheza chini na kushambulia kwa kushtukiza ingawa kitu kizuri wamepata ushindi muhimu.
“Tulicheza, tuliutawala mchezo lakini tukashindwa kutengeneza nafasi za kutosha za kufunga lakini ndio mpira, tunarudi kujipanga kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa makundi.
“Binafsi sijaja kwenye mashindano haya kuangalia matokeo, nimekuja kuangalia viwango vya wachezaji wangu pia nimetoa nafasi kwa wachezaji vijana, wamenishangaza kwa jinsi walivyocheza kwenye timu kubwa kama Yanga,” alisema Gamondi.
“Tunapaswa kupongeza kwa kile kinachofanyika, wachezaji wamecheza vizuri wamejaribu kuonesha kiwango kizuri licha ya kucheza mfululizo,” alisema Gamondi.