London, England
Kipigo cha mabao 2-1 ilichokipata Arsenal mbele ya Fulham kimeifanya timu hiyo kuuanza vibaya mwaka mpya 2024 kwa kushuka hadi nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England (EPL) ingawa kocha Mikel Arteta amepuuza mpango wa kusajili mchezaji mwingine.
Fulham ilineemeka kwa mabao ya Jimenez na De Cordova-Reid wakati bao pekeel la Arsenal likifungwa na Bukayo Saka hali ambayo imeibua wasiwasi juu ya uwezo wa wachezaji wa Arsenal kwenye mbio za taji la EPL.
Arteta hata hivyo amesema kinachotakiwa kufanywa na timu hiyo kwa sasa si kusajili wachezaji wapya badala yake kufanya kile walichokuwa wakikifanya katika mechi 19 zilizopita.
“Tunatakiwa kufanya kile tulichokifanya katika mechi 19 za nyuma ,” alisema Arteta jana Jumapili mara baada ya timu yake kupoteza mechi hiyo ambayo katika EPL ni mechi yao ya 20.
Kauli ya Arteta imekuja wakati huu dirisha dogo la usajili likiwa wazi na kocha huyo amejikuta katika presha ya kutakiwa kufanya usajili ili kujiimarisha katika mbio za kulitwaa taji la EPL msimu huu.
Kabla ya mechi hiyo ya jana, Arsenal pia ilipoteza mechi nyingine ya EPL Alhamisi iliyopita kwa mabao 2-0 dhidi ya West Ham hali ambayo pia iliibua wasiwasi kwamba huenda timu hiyo haina uwezo tena wa kulipigania taji.
“Siku tatu zilizopita tulipoteza mechi ambayo kimsingi ilikuwa mechi yetu ya kushinda, leo (jana) imekuwa mechi mbaya mno ya msimu wetu,” alisema Arteta.
“Kama tutacheza kama tulivyocheza mechi nyingine 19 zilizopita tutapanda juu katika ligi, lakini kama tutacheza kama tulivyocheza leo (jana) hatufiki popote, ni siku ngumu ‘kumeza’,” alisema Arteta.
Liverpool ambayo inaonekana kwa sasa ndiye mpinzani mkuu wa Arsenal katika mbio za kuliwania taji la EPL msimu huu, leo Jumatatu itaumana na Newcastle, ikishinda mechi hiyo itajiimarisha kileleni na kuiacha Arsenal kwa tofauti ya pointi tano.
