Na mwandishi wetu
Yanga, leo Jumatano jioni imetakata kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya kuilaza Real Bamako ya Mali mabao 2-0 katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ushindi huo umeifanya Yanga kujiweka pazuri katika mbio za kuelekea robo fainali ikiwa nafasi ya pili katika kundi hilo na pointi saba baada ya kucheza mechi nne kama timu nyingine za kundi hilo.
US Monastir ya Tunisia inashika usukani wa kundi hilo, ina pointi 10 wakati TP Mazembe ya DR Congo inashika nafasi ya tatu na ina pointi tatu na Real Bamako inaburuza mkia na pointi zake mbili.
Yanga ilipata bao lake la kwanza katika dakika ya nane ya mchezo huo mfungaji akiwa Fiston Mayele ambaye aliukokota vyema mpira kabla ya kuujaza wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake.
Kama kawaida yake baada ya kufunga bao hilo, Mayele aliwasogelea mashabiki jukwaani akiwa pamoja na wachezaji wenzake na kushangilia kwa staili ya kutetema huku mashabiki wakimuunga mkono.
Dakika ya 68 Yanga iliandika bao la pili lililofungwa na Moloko ambaye aliyatumia vizuri makosa ya beki wa Mali aliyejichanganya akiwa na mpira. Moloko baada ya kuunasa mpira huo aliukokota na kukimbia nao kwa kasi kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Yanga hata hivyo itabidi ijilaumu kwa kushindwa kuzitumia nafasi kadhaa kupata bao, mfano dakika ya 55, Mayele aliangushwa ndani ya eneo la 18 na mwamuzi kuipa timu hiyo penalti.
Wachezaji wa Real Bamako waliilalamikia penalti hiyo lakini marudio ya picha ya video yalionesha ilikuwa penalti wazi. Bangala aliyekabidhiwa jukumu la kupiga penalti hiyo, shuti lake lilipaa juu ya lango.
Dakika ya 43 Mayele akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga baada ya kuinasa krosi alipiga mpira wa kichwa ambao ulikwenda nje ya lango.
Dakika mbili baadaye, Mayele tena akiwa katika nafasi nzuri aliiwahi krosi na kuunganisha kwa shuti la mguu wa kulia ambalo pia lilitoka nje.
Real Bamako pamoja na kipigo hicho lakini hawakumuacha katika utulivu kipa wa Yanga, Diarra ambaye walimpelekea mashambulizi ya mara kwa mara lakini wakati wote alikuwa makini kulilinda lango lake.
Diarra aliibua hofu kwa mashabiki wa Yanga baada ya kugongana na mchezaji mmoja wa Bamako na kulala chini ambapo ilibidi watu wa husuma ya kwanza waitwe baada ya kipa huyo kuanza kutema damu lakini baadaye alii ya kuhudumiwa aliinuka na kuendelea na mchezo.
Kocha wa Yanga, Nabi alifanya mabadiliko kadhaa kwa kuwatoa Bangala na kumuingiza Mauya, Moloko na kumuingiza Mzize na Aziz Ki ambaye nafasi yake aliingia Aucho.
Kimataifa Yanga yatakata Kwa Mkapa
Yanga yatakata Kwa Mkapa
Read also