Na mwandishi wetu
Kikosi cha timu ya Yanga kinatarajia kukwea pipa keshokutwa Jumanne alfajiri na Jumatano kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad.
Timu hiyo inaondoka kwa mafungu wakianza wachezaji waliokuwa wakijifua Avic Town, Dar es Salaam kisha Jumatano wataondoka wachezaji walio kwenye majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars wanaotarajia kukipiga Jumanne dhidi ya Morocco.
Wachezaji wengine waliokuwa kwenye timu zao za taifa; Stephane Aziz Ki wa Burkina Faso, Khalid Aucho (Uganda) na kipa Djigui Diarra (Mali) nao watajiunga na kikosi hicho Algeria baada ya kumaliza majukumu yao.
Taarifa hiyo ambayo imewekwa wazi leo Jumapili na ofisa mmoja wa timu hiyo ambaye hakutaka kuandikwa jina mtandaoni kwa kuwa si msemaji wa timu hiyo alieleza kuwa kikosi kinatarajia kuondoka majira ya saa 11 alfajiri.
“Wachezaji wengine waliokuwa na Taifa Stars wao wataondoka siku inayofuata na kina Aziz Ki na Aucho wao watatokea Morocco wanakocheza mechi zao na kwenda Algeria lakini Diarra yeye atatoka Mali na kujiunga na timu na kukamilisha kikosi kamili dhidi ya Belouizdad,” alieleza ofisa huyo.
Yanga inatarajia kuumana na Belouizdad katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi Novemba 24, mwaka huu mjini Algiers.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amenukuliwa akisema kuwa anakiamini kikosi chake kuelekea mechi hizo za makundi kutokana na mipango waliyoisuka kuhakikisha wanafika mbali katika michuano hiyo msimu huu waliyorejea kushiriki baada ya miaka 25.