Saudi Arabia
Cristiano Ronaldo jana Alhamisi aliifungia Al Nassr mabao manne katika mechi ya ligi dhidi ya Al Wehda, hapo hapo akaweka rekodi ya kufunga mabao 500 katika klabu mbalimbali alizochezea hadi sasa.
Winga huyo wa zamani wa Man United na Real Madrid, alifunga mabao hayo pekee kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa King Abdulaziz na Al Nassr kutoka na ushindi wa mabao 4-0.
Ronaldo ambaye ana miaka 38 sasa, alifunga bao la kwanza dakika ya 21 na kuwa bao lake la 500 katika klabu mbalimbali kabla ya kuongeza mengine matatu likiwamo moja la penalti na hivyo kufikisha jumla ya mabao 503.
Desemba mwaka jana Ronaldo alivunja mkataba na Man United na kusaini mkataba na Al Nassr ya Saudi Arabia, mkataba utakaofikia ukomo mwaka 2025 huku ikidaiwa kuwa kwa mwaka analipwa Dola 75 milioni.
Baada ya kucheza mechi mbili za Al Nassr bila bao, hatimaye alifunga bao moja na sasa ameongeza mabao mengine manne na hivyo kufikisha idadi ya mabao matano tangu ajiunge na timu hiyo.
Kwa ushindi huo, Al Nassr sasa inashika usukani wa ligi hiyo kubwa nchini Saudi Arabia ikiwa imecheza mechi 16 na ina pointi 37 sawa na Al Shabab zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa huku Al Shabab ikicheza mechi 17 wakati Al Nassr imecheza mechi 16.
Kimataifa Ronaldo aweka rekodi ya mabao 500
Ronaldo aweka rekodi ya mabao 500
Read also