Beverly Hills, Marekani
Rais wa Fifa, Gianni Infantino kwa mara nyingine ametetea bei ya tiketi kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 na kupuuza hoja kwamba tiketi ya mechi ya fainali imeuzwa tena kwa bei ya zaidi ya dola 2 milioni.
Akiwa mjini Beverly Hills hivi karibuni, Infantino alizungumzia malalamiko yanayoelekezwa Fifa kuhusu bei kubwa ya tiketi kwa mechi za fainali hizo ambapo amedai kuwa gharama hizo zinahusu soko la Marekani.
Fainali za Fifa za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 mwaka huu.
fifa imekuwa ikilalamikiwa na kutuhumiwa kwa ulaghai kuhusu gharama za tiketi lakini Infantino amesisitiza kuwa mapato yatakayopatikana kwenye fainali hizo yatasaidia maendeleo ya soka duniani kote.
Mashabiki pia wamekuwa wakiulalamikia uongozi wa Fifa kwa kutenga maeneo ya tiketi za bei mbaya ambapo sehemu kubwa ya tiketi zimewekwa kwa mashabiki wanaomudu maeneo hayo ya gharama za juu.
“Ni lazima tuliangalie soko, tuko katika soko ambalo duniani kote wao kwenye burudani wamepiga hatua kubwa, kwa hiyo ni lazima tuangalie hadhi ya soko hilo,” alisema Infantino.
Infantino alifafanua kuwa nchini Marekani kuna ruhusa ya kuongeza bei ya tiketi kwa mara ya pili na hivyo kama utauza tiketi kwa bei ya chini una haki ya kuongeza bei na kuuza kwa bei ya juu.
Aliongeza kuwa ingawa kuna wanaolalamikia bei ya Fifa ya tiketi kuwa kubwa lakini watu hao hao ndio wanaokwenda kuzinunua tiketi hizo katika masoko mengine kwa zaidi mara mbili ya bei ya Fifa.
