Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG ya Ufaransa na timu ya Taifa ya Brazil, Neymar amedokeza kuwa huenda fainali za Kombe la Dunia za Qatar zikawa za mwisho kwake kuiwakilisha Brazil kwa kuwa haijui hatma yake katika michuano ijayo.
Neymar mwenye umri wa miaka 30, amewahi kuiwakilisha Brazil katika michuano miwili iliyopita ya Kombe la Dunia yaani mwaka 2014 na 2018 na hajawahi kubeba taji hilo na sasa amesema kwamba atacheza katika fainali za Qatar kama ndio za mwisho kwake.
“Nitacheza kama fainali zangu za mwisho, nimezungumza na baba yangu, huwa tunazungumza kila wakati, tumezungumza kuhusu kucheza kama vile hizi ni fainali za mwisho kwa sababu hujui nini kitatokea kesho,” alisema Neymar.
“Siwezi kujihakikishia kama nitacheza tena kwenye Kombe la Dunia, ukweli ni kwamba sifahamu, hivyo nitacheza katika michuano hii kama ni ya mwisho kwangu, labda nitacheza michuano mingine, itategemea, kutakuwa na mabadiliko ya mkocha na sijui kama kocha huyo atapenda kuwa na mimi,” alisema Neymar.
Kocha wa sasa wa Brazil, Tite ataachana na timu hiyo mara baada ya fainali za Kombe la Dunia za Qatar ambazo zitaanza kutimua vumbi Novemba 20 na mrithi wake bado hajatangazwa. Brazil inajivunia rekodi ya kubeba taji la dunia mara tano na kwa mara ya mwisho ilibeba taji hilo mwaka 2002.
Neymar aliyeanza kuichezea Brazil akiwa na miaka 18, alisema kwamba amejitahidi kujenga historia nzuri katika timu ya Taifa na angependa kumaliza vizuri katika timu hiyo.
Kimataifa Neymar: Qatar ndio mwisho wangu
Neymar: Qatar ndio mwisho wangu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
