Mwandishi wetu, Arusha
Yanga leo imezianza mbio za Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2022/23 kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania ikineemeka kwa mabao ya Fiston Mayele na Bakari Nondo Mwamnyeto.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid jijini hapa, Polisi ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Yanga kwa bao lililopatikana dakika 10 kabla ya timu kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Salum Kipemba.
Bao hilo lilionekana kuibua matumaini kwa Polis kuwasimamisha Yanga kabla ya matumaini hayo kupotea dakika nane baadaye Yanga waliposawazisha kupitia kwa Mayele aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Shaban Djuma ambaye mpira wake wa kona uliunganishwa kwa kichwa na Mwamnyeto kabla ya kuokolewa na kipa wa Polisi na kisha kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Timu hizo zilikianza kipindi cha pili kwa kushambuliana kwa zamu lakini zikiwa zimebaki dakika tano mpira kumalizika alikuwa ni Mwamnyeto aliyeihakikishia Yanga pointi tatu muhimu baada ya kuandika bao la pili akiitumia vizuri kona ya Benard Morrison.
Mayele, mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita itabidi ajilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na mabao mawili baada ya kukosa penalti iliyotolewa baada ya Shaban Stambuli kumuangusha Jesus Moloko katika eneo la hatari lakini umahiri wa kipa wa Polisi, Kelvin Igenderezi ulitosha kuwa kikwazo kwa Mayele kuipatia Yanga bao.
Ushindi huo unakuwa mwanzo mzuri kwa Yanga pamoja na Mayele ambaye bila shaka anakuwa amezianza mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora wa ligi, tuzo ambayo alishindwa kuibeba msimu uliopita akizidiwa na George Mpole wa Geita Gold aliyemaliza ligi na mabao 17 akimzidi Mayele kwa tofauti ya bao moja.
Baada ya mchezo huo Yanga itaingia dimbani Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tena kuumana na Coastal Union, katika mechi inayotarajiwa kuwa ngumu kwa timu zote mbili. Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi kati ya KMC na Coastal, Simba itaivaa Geita na Azam kuumana na Kagera Sugar. Katika mechi nyingine za ligi hiyo iliyochezwa leo, Singida Big Stars iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Ligi kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons.
.
