Geneva, Switzerland
Maofisa wa soka wa Iran watafanya kikao na wenzao wa Fifa katika siku za karibuni kwa lengo la kuweka sawa mipango ya mechi za Iran kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza mwezi ujao nchini Marekani.
Bosi wa Shirikisho la Soka Iran, Mehdi Taj amesema wana mambo ya kujadili baada ya kurudi nyumbani akiwa ameshindwa kushiriki mkutano mkuu wa mwaka wa Fifa uliofanyika Alhamisi Aprili 30, 2026 mjini Vancouver, Canada.
Katibu Mkuu wa Fifa, Mattias Grafström amewaalika maofisa wa soka nchini Iran kukutana nao katika makao makuu ya Fifa mjini Zurich, kikao ambacho kinatarajia kufanyika Mei 20, 2026 au kabla ya hapo.
Lengo ni kuhakikisha kikao hicho kinafanyika wiki tatu kabla timu ya Iran haijawasili Marekani kuweka kambi ya mazoezi mjini Arizona na kujiandaa na mechi tatu za makundi zitakazochezwa Seattle, California na Inglewood.
“Msimamo wetu ni kwamba hivi karibuni tutakuwa na kikao na watu wa Fifa,” alisema Taj katika mazungumzo yake na chanzo kimoja cha habari nchini Iran.
Awali Rais wa Fifa, Gianni Infantino katika hotuba yake ya ufunguzi mbele ya viongozi wa soka duniani isipokuwa wa Iran, alisisitiza Iran itacheza mechi za Kombe la Dunia nchini Marekani kama ilivyopangwa.
Kauli hiyo ilifuatiwa na kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye alithibitisha kuiunga mkono timu ya Iran na kuongeza kuwa kama Infantino hana tatizo na yeye Trump hana tatizo ingawa awali Trump alisema anaikaribisha Iran lakini hawezi kuihakikishia usalama.
Katika hoja ya awali, Iran walitaka mechi zao zisichezwe nchini Marekani, hoja ambayo hata hivyo haikuungwa mkono na Rais wa Fifa ambaye amekuwa na ukaribu na Rais Trump katika miezi ya karibuni na amewahi kumpa tuzo kiongozi huyo wa Marekani jambo lililoibua mjadala..
Tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kumekuwa na mgogoro mkubwa kuhusu hatma ya timu ya taifa ya Iran kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwezi ujao katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
