Na mwandishi wetu
Simba imeichapa Coastal Union mabao 4-0 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania, ushindi ambao umeiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi, Juni 20, 2026, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Simba ilitawala karibu kila eneo na haikushangaza kutoka uwanjani na ushindi huo mnono.
Coastal ilianza kwa kuonesha uhai lakini hali ilianza kuwa tete katika dakika ya 20 ilipoanza kunyanyaswa kwa bao lililofungwa na Libasse Gueye na kudumu hadi mapumziko.
Simba iliendelea kuonesha uhai katika kipindi cha pili cha mchezo huo, dakika 10 baada ya kuanza kipindi hicho, Nickson Kibabage aliwainua vitini mashabiki alipoifungia timu hiyo bao la pili.
Coastal licha ya kujipanga na kutengeneza mashambulizi kadhaa kwa lengo la kusaka bao la kwanza lakini walikuwa ni Simba waliofanikiwa kuongeza bao la tatu lililofungwa na Rushine De Reuck katika dakika ya 77.
Zikiwa zimebakia dakika tatu kabla ya kumalizika kwa mchezo huo, Clatous Chama alikamilisha hesabu za Simba kwa kuifungia timu hiyo bao la nne.
Kwa ushindi huo Simba inasubiri kuumana na mshindi wa mechi ya Yanga na Azam FC itakayopigwa Jumapili Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Soka Simba yaipiga Coastal 4-0 Kombe la Shirikisho
Simba yaipiga Coastal 4-0 Kombe la Shirikisho
Related posts
Read also
