Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema msimu huu wa 2023-24 timu yake itabeba taji la Ligi Kuu England (EPL) na hivyo kuweka rekodi ya kulibeba taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.
Pep ametoa kauli hiyo wakati timu yake inashika nafasi ya nne katika EPL baada ya kutoa sare katika mechi dhidi ya Chelsea, Liverpool na Tottenham.
“Kwa fikra zangu ni kwamba tunakwenda kubeba taji la ligi kuu, kama tutacheza kwa kiwango kile tulichocheza katika mechi dhidi ya Liverpool na Tottenham, tunakwenda kubeba taji kwa mara nyingine,” alisema Pep.
Kocha huyo alisema kwamba watu hawaamini baada ya kupata sare tatu lakini wakiangalia wanaona wanabeba taji kwa mara nyingine na wanafahamu kwamba si jambo rahisi kwa sababu hakuna timu iliyowahi kufanya hivyo (kubeba taji mara nne mfululizo).
“Ugumu upo pale pale na ulikuwapo msimu uliopita lakini kama utaniuliza leo ninavyoona hali, yaani tunakwenda kubeba taji kwa mara nyingine,” alisema Pep.
Kauli ya Pep inaweza kukumbusha tukio la msimu uliopita baada ya timu hiyo kuwa nyuma ya Arsenal kwa tofauti ya pointi nane lakini mwishowe wakafanikiwa kubeba taji la ligi hiyo.
Mechi dhidi ya Tottenham iliyoisha kwa sare ya mabao 3-3 ilimsababishia matatizo mwamuzi Simon Hooper ambaye alizongwa na wachezaji wa Man City wakimlaumu kwa kuwapa mpira wa adhabu wakati ilitakiwa aache mchezo uendelee (advantage) kwani walikuwa wameuwahi mpira.
Arsenal kwa sasa ndiyo inayoshika usukani wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi saba ikiwa imecheza mechi 15 ikifuatiwa na Liverpool yenye pointi 31 na leo itacheza mechi ya 15 dhidi ya Sheff United.
