Juventus, Italia
Kiungo wa Juventus, Paul Pogba ameeleza kushtushwa na kusikitishwa baada ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa miaka minne kwa kosa la kutumia madawa ya kusisimua misuli.
Pogba, 30, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa alisimamishwa kujihusisha na soka Septemba mwaka jana baada ya vipimo vya awali kubaini kuwa mwili wake ulikuwa na madawa hayo.
“Kila kitu nilichokifanikisha katika maisha yangu ya soka nimeporwa,” alisema Pogba katika taarifa yake na kusisitiza kwamba anakusudia kukata rufaa.
Pogba alifanyiwa vipimo vya ghafla Agosti 20 mwaka jana mara baada ya mechi ya kwanza ya Juventus ya msimu wa 2023-24.
Vipimo hivyo baadaye vilithibitishwa na Tume ya Kudhibiti Madawa (Nado) nchini Italia katika vipimo vya mara ya pili vilivyofanywa Oktoba na waendesha mashtaka wa Nado kuomba afungiwe miaka minne.
Pogba alisema kwamba anaamini matokeo ya vipimo hivyo hayakuwa sahihi na hakuwahi kufahamu kama amewahi kutumia dawa za kuongea nguvu kwa makusudi au kwa kutojua.
“Baada ya kumaliza vikwazo nilivyowekewa kisheria habari kamili itakuwa wazi,’ alisema Pogba na kusisitiza kuhusu nia yake ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhisho ya Michezo (Cas).
Wakala wa Pogba, Rafael Pimenta alisema kwamba jambo pekee ambalo ana uhakika nalo ni kwamba mchezaji huyo hakuwahi kutaka kuvunja sheria.
Pogba ambaye pia aliwahi kukipiga Man United, akiwa Juventus mshahara wake kwa mwaka ulikuwa Pauni 6.8 milioni lakini tangu asimamishwe Septemba mwaka jana, pato hilo lilishuka na kuishia Pauni 2,054 kwa mwezi.