Na mwandishi wetu
Baada ya Simba Queens, Yanga Princess kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake jana Alhamisi, makocha wa timu hizo wamekiri kuwa ubora wa vikosi vyao uliamua matokeo hayo.
Mechi hiyo iliyopigwa jana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Chioma Wogu kwenye kipindi cha kwanza kabla ya Vivian Aquino kusawazisha kipindi cha pili.
Kocha wa Princess, Sebastian Nkoma alisema kuwa mchezo ulikuwa mzuri na walijiandaa kupata matokeo ila wamekutana na mpinzani mzuri mwenye uzoefu na kikosi kipana.
“Mechi ilikuwa nzuri, timu zote zina uwezo mkubwa, Simba wana uzoefu na wana kikosi kikubwa mimi bado watoto wangu hawana uzoefu ila naendelea kuwaandaa naamini watakuwa bora baadaye,” alisema Nkoma aliyeondoka Simba Queens msimu uliopita.
Alisema Simba inayoonekana aliiandaa yeye na kwamba kama angepata muda zaidi wa kuiandaa Yanga Princess kwa zaidi ya wiki tatu basi wapinzani wake wasingetoka salama lakini kwa bahati mbaya Wekundu hao walimuwahi .

Kwa upande wake Kocha wa Queens, Charles Lukula alisema mpira umekuwa mzuri sana na kwamba alijua wazi haitakuwa rahisi kwa kuwa wapinzani wao pia, wana kikosi kizuri na chenye kupambana ingawa aliwashukuru wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kusawazisha bao baada ya kutanguliwa na Yanga.
“Kila timu inataka kombe, kila timu imepata wachezaji wazuri na inataka ushindi kwa hiyo kila anayekuja amejiandaa kupambana na ndicho kilichotokea leo (jana), mechi imekuwa na ushindani mkubwa,” alisema Lukula.
Hiyo ni mechi ya tatu kwa timu hizo tangu kuanza kwa ligi msimu huu ambapo kabla ya kukutana jana kwenye mechi ya kwanza wote walipoteza kabla ya kila timu kushinda mabao 4-0 kwenye mechi za pili za ligi hiyo.
