Na mwandishi wetu
Baada ya kuifumua Ihefu mabao 2-0, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kilichowapa ushindi ni kusoma udhaifu wa wapinzani wao na kuwabana katika dakika zote 90 za mchezo huo.
Kagera ilipata ushindi huo kwenye mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza siku tatu zikiwa zimepita tangu Ihefu itoke kuifunga Yanga mabao 2-1 Jumanne iliyopita na kumaliza ubabe wa Yanga wa kutofungwa mechi 49 mfululizo.
Maxime alieleza kwamba kwanza hakuangalia matokeo ya Ihefu yaliyopita isipokuwa aliitazama timu hiyo kwa mapungufu na uzuri wao wa kikosi na kisha akaweka mbinu zake na hatimaye kufanikiwa kuondoka na pointi tatu.
“Tunashukuru tunaendelea kupata ushindi, kikubwa tumeikuta timu iko vibaya na sasa inaendelea kukaa vizuri, tunahitaji iendelee kubaki hivi katika siku za usoni ili tufikie malengo tuliyonayo.
“Kiujumla sikutazama Ihefu imeshinda dhidi ya nani, mimi niliwaangalia wao na kisha nikaweka mbinu zangu, walianza vizuri kiushindani lakini baadaye walirudi chini, sikujua walikuwa na mpango gani lakini ukatumika mwanya huo kuwamaliza,” alisema Maxime.
Kagera imekuwa na mwenendo mzuri hivi karibuni baada ya kuibuka na ushindi wa mechi tatu, sare moja na kufungwa moja katika mechi tano za mwisho ikikamata nafasi ya sita kwa pointi 21 baada ya mechi 15.
Soka Maxime ataja kilichoikwaza Ihefu
Maxime ataja kilichoikwaza Ihefu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
