Na mwandishi wetu
Wachezaji watatu wa Simba, kipa Aishi Manula, beki Shomari Kapombe na kiungo Clatous Chama wamerejea kwenye mazoezi ya timu hiyo kujiandaa na mechi yao ya Jumamosi hii dhidi ya Yanga.
Awali, taarifa za kuumia kwa wachezaji hao siku chache kabla ya mechi yao ngumu dhidi ya Yanga ziliibua hofu kubwa lakini sasa wamerejesha matumaini kwa mashabiki wa Wekundu hao kutokana na kurejea kwao kikosini mapema.
Manula na Kapombe waliumia kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya Geita Gold waliyotoka sare ya bao 1-1 wakati Chama inaelezwa kuwa alijitonesha goti lake kwenye mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Yanga.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amefafanua kuwa Manula ameanza mazoezi na wachezaji wengine tangu Jumatatu akisubiri kukauka kwa majeraha yake ya vidole ili aanze mazoezi ya ugolikipa.
“Manula yeye ambaye aliumia na kioo kabla ya kuanza kwa mchezo na Geita anaendelea vizuri akifanya mazoezi na wenzake akisubiri kukauka kwa vidonda vyake vya vidoleni ili aanze mazoezi ya ukipa mapema.
“Kapombe ambaye naye aliumia nyama za paja juzi (Jumatatu) na jana (Jumanne) alikuwepo mazoezini anaendelea vizuri kabisa na tunatarajia pengine leo ataanza na wenzake kwenye ratiba za usoni zaidi,” alisema Ally.
Kuhusu Chama, Ally alieleza kwamba mchezaji huyo ameanza mazoezi mepesi aliyofanya kwa siku mbili mfululizo na hivyo anatarajia kujiunga kwenye mezoezi ya moja kwa moja na wenzake akiwa na uwezekano mkubwa pia wa kutumika kwenye mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Azam (ASFC) itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Wakati Simba ikiwa Mwanza kujiandaa na mchezo huo, Yanga yenyewe ipo Shinyanga ikiendelea kujifua kwa ajili ya mchezo huo wa tatu kukutana timu hizo ndani ya msimu huu, wakitafuta nani mbabe baada ya mechi mbili za ligi za awali kuisha kwa suluhu.
Soka Kapombe, Chama, Manula warejesha matumaini
Kapombe, Chama, Manula warejesha matumaini
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
