Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema kurejea kikosini kwa walinzi; Abdallah Sebo na Daniel Amoah kumeongeza uimara kwenye safu yake ya ulinzi.
Nyota hao wawili walikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakiuguza majeraha ambapo Sebo alifanyiwa upasuaji mdogo wa goti wakati Amoah alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu.
“Wamekuja muda sahihi kuongeza ubora katika ulinzi, ni wakati mwafaka ambao tunahitaji kuwa bora ili kupata ushindi utakaotuweka karibu na malengo yetu ambayo ni ubingwa msimu huu,” alisema Dabo.
Dabo raia wa Senegal alisema wachezaji hao wana uzoefu mkubwa na ligi ya Tanzania hivyo mchango wao katika kipindi hiki ni muhimu sababu hawapo tayari kuona wanapoteza mchezo kutokana na malengo waliyonayo msimu huu.
Alisema anatambua ushindani uliopo kwenye ligi na timu yake imeruhusu mabao 16 msimu huu lakini watapambana kuhakikisha wanacheza kwa tahadhari ili kuhakikisha hawadondoshi pointi katika mechi zao tisa zilizobaki.
Azam ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi 45 katika michezo 21 huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa kileleni kwa pointi 52 na michezo 20.
Soka Sebo, Amoah kuimarisha ulinzi Azam
Sebo, Amoah kuimarisha ulinzi Azam
Read also