Na mwandishi wetu
Baada ya Tanzania Prisons kutoa sare ya bao 1-1 juzi dhidi ya Geita Gold, imeeleza kuwa wamepata nguvu ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi zao nne zilizobaki kuhakikisha wanasalia Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Kauli hiyo imetolewa na mshambuliaji mkongwe wa timu hiyo, Jeremiah Juma ambaye alifunga bao kwenye mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kusisitiza kuwa sasa amerejea kwenye makali yake.
“Tumebakiza mechi nne dhidi ya KMC, Azam, Simba na Ruvu Shooting na zote tunataka matokeo na wanajua kwamba tunahitaji kweli ushindi, tuna imani mchezo mgumu kwetu utakuwa dhidi ya Ruvu Shooting lakini tutapambana kuhakikisha tunasalia Ligi Kuu, tunajua tunaweza kulitimiza hilo.
“Nashukuru pia nimefunga kuisaidia timu yangu kupata angalau pointi moja. Muda mrefu sijafunga na huwa inatokea lakini sasa nimeanza tena naamini nitafunga kwenye mechi hizi nne zilizobaki, lengo ni kuisaidia timu isishuke daraja,” alisema Juma aliyefunga mabao sita mpaka sasa.
Prisons inashikilia nafasi ya 14 kwa pointi 25 ikizizidi pointi moja timu mbili za mwisho, Biashara United na Mbeya Kwanza zenye pointi 24 kila moja. Katika mechi nne zilizosalia, mechi tatu Prisons itacheza ugenini na moja dhidi ya Simba watakipiga kwao Sokoine.
Soka Sare yaipa nguvu Prisons
Sare yaipa nguvu Prisons
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
