Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumanne imepata ushindi mwingine wa pili katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuilaza Coastal Union ya Tanga mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 28 lililofungwa na Fiston Mayele ambaye aliunganisha kwa kichwa krosi ya Lomalisa na mpira kugonga mwamba kabla ya kumrudia tena Mayele aliyeusukumiza wavuni kwa shuti hafifu akiwa karibu kabisa na lango la Coastal.
Dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili, Mayele akaandika bao la pili la Yanga safari hii akiitumia pasi ya Aziz Ki aliyekokota mpira akiwa karibu na eneo la kati kabla ya kumtangulizia mfungaji aliyefumua shuti la chinichini na mpira kumshinda mlinda mlango wa Coastal, Mahmoud.
Feisal Salum au Fei Toto aliwainua vitini mashabiki wa Yanga katika dakika ya 65 alipoandika bao la tatu akiuwahi mpira uliokuwa ukikokotwa na Azizi Ki uliotokana na pasi ya Moloko. Wakati Aziz Ki akikokota mpira huo na mguu wake wa kushoto, Fei Toto aliyekuwa kwenye kasi akauvuta na kufumua shuti lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni.
Kwa ushindi huo Yanga inaendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa imefikisha pointi 44 katika jumla ya mechi 17 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37 katika mechi 16 kama Azam ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36.
Ushindi wa leo haukuwa na maana kubwa kwa Yanga tu bali hata Mayele ambaye ameendelea kuimarisha rekodi yake ya mabao na kufikisha jumla ya mabao 13 akiwa ameshika usukani akizidi kumkimbia Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10 anayeshika nafasi ya pili wakati Fei Toto naye akiendelea kupambana akiwa amefikisha mabao sita hadi sasa.
Kwa upande mwingine matokeo hayo yanakuwa mwanzo mbaya kwa kocha wa Coastal, Joseph Lazaro ambaye ndio mechi yake ya kwanza akiwa amekabidhiwa majukumu ya kocha Yusuph Chippo kutoka nchini Kenya ambaye mkataba wake ulisitishwa jana na uongozi wa Coastal.
Coastal hadi sasa inashika nafasi ya 13 katika mechi 17 ikiwa imejikusanyia pointi 15 hali ambayo inazidi kuibua wasiwasi kuhusu mambo ya baadaye ya timu hiyo kwenye ligi.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, Ruvu Shooting na Kagera Sugar zilitoka sare ya bila kufungana.
Soka Yanga yaitandika Coastal 3-0
Yanga yaitandika Coastal 3-0
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
