Na mwandishi wetu
Yanga imechapwa bao 1-0 na AS FAR Rabat ya Morocco katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi iliyochezwa Jumamosi Februari 7, 2026, matokeo yanayofifisha matumaini ya timu hiyo kufuzu robo fainali ingawa kimahesabu nafasi bado ipo.
Bao lililoizamisha Yanga lilipatikana dakika ya 85 mfungaji akiwa ni Anas Bach ambaye aliuwahi mpira na kufumua shuti la mguu wa kulia lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni.
Yanga iliyokuwa ugenini ilionesha uhai kwa dakika zote 90 za mchezo na mara kadhaa ililikaribia lango la AS Rabat na hata baada ya kufungwa, juhudi za kusaka bao la kusawazisha zilikuwa vile vile ingawa hazikuzaa matunda.
Kwa matokeo hayo Yanga imeshuka hadi nafasi ya tatu katika Kundi B ikibaki na pointi tano nyuma ya vinara Al Ahly wenye pointi tisa na tayari wamefuzu wakifuatiwa na AS Rabat wenye pointi nane.
JS Kablye ya Algeria inashika mkia na pointi zake tatu katika kundi hilo na katika mechi yake na Ahly ilitoka sare ya bila kufungana.
Kwa jinsi hesabu zilivyo Yanga watahitaji kushinda mechi yao ya mwisho dhidi ya JS Kabylie ya Algeria lakini ushindi pekee hautoshi bali pia timu hiyo itahitaji kuombea Rabat wapoteze mchezo wao wa mwisho na Ahly.
Matokeo ya sare kati ya Yanga na JS Kablye yatakuwa yameitoa Yanga katika mashindano hayo na hiyo maana yake ni kwamba Yanga inahitaji kushinda huku ikiombea AS Rabat nayo ishindwe.
Tofauti ya mabao katika mechi hizo za mwisho pia ina maana kubwa kwani licha ya Yanga kuhitaji ushindi ili ifikishe pointi nane ambazo tayari AS Rabat wanazo bado idadi ya mabao watakayofungwa AS Rabat pia ina maana kubwa kwa Yanga.
Kadri AS Rabat watakavyofungwa mabao mengi ndivyo Yanga itakapokuwa na nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.
Kimataifa Yanga yaIala Morocco, matumaini yafifia
Yanga yaIala Morocco, matumaini yafifia
Read also
