Mainz, Ujerumani
Winga Anwar El Ghazi (pichani) aliyetimuliwa na klabu ya Mainz 05 ya Ujerumani ametangaza kuchukua hatua za kisheria juu ya uamuzi huo akidai kwamba ametimuliwa kimakosa.
Novemba 2 mwaka huu, klabu ya Mainz ilitangaza kuvunja mkataba na El Ghazi baada ya mchezaji huyo kutumia mitandao ya kijamii kuweka maandiko yaliyohusu mgogoro wa Israel-Gaza.
“Sioni taarifa yoyote katika maandiko niliyoyaweka mitandaoni ambayo haiendani na uhuru wa kutoa maoni,” ilieleza taarifa ya mchezaji huyo kupitia mawakili wake ambao wanalifikisha suala hilo mahakamani.
Klabu ya Mainz ilikiri kupewa taarifa na wanasheria wa mchezaji huyo kuhusu uamuzi wa kupinga kutimuliwa na klabu hiyo ingawa klabu hiyo ilikataa kusema lolote kwa madai kwamba suala hilo kwa sasa ni la kisheria.
Mwezi uliopita El Ghazi, 28, alisimamishwa na klabu ya Mainz kutokana na maandiko yake ya kwenye mitandao ya kijamii yakiwamo maandiko ambayo yametafsiriwa kuwa yanazungumzia kuangamizwa kwa Israel.
Baada ya kusimamishwa, El Ghazi, alitishiwa na klabu hiyo kwamba ingemfutia mkataba lakini alirudishwa katika kikosi cha timu hiyo siku chache baadaye na hapo hapo akasema kwamba anasimamia amani kuliko kitu chochote.
Mainz mara baada ya kumrudisha mchezaji huyo ilitoa taarifa iliyodai kwamba El Ghazi ameendeleza utaratibu wa klabu hiyo wa kuyatumia makosa kama fursa ya kujifunza lakini mwenyewe akaibuka na kudai kwamba hakuiruhusu klabu hiyo kutoa taarifa hiyo na hawezi kujitenga na kile alichokisema.
“Siwezi kujitenga na kile nilichokisema na nitaendelea kusimamia ubinadamu na kutetea kundi la wanaokandamizwa hadi pumzi yangu ya mwisho,” alisema El Ghazi.
Kauli hiyo iliufanya uongozi wa Mainz kumfutia mkataba uamuzi ambao umemuibua upya akidai kwamba anaupinga kisheria lakini pia akasema kwamba ataendelea kusimamia haki hata kama atabaki peke yake.