Manchester, England
Manchester City imekamilisha usajili wa beki wa kati wa nguvu, Josko Gvardiol (pichani) kutoka Leipzig ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 77 milioni na mkataba wa miaka mitano.
Josko, ambaye pia ni beki wa timu ya Taifa ya Croatia anakuwa beki wa pili kuuzwa bei mbaya baada ya Harry Maguire aliyesajiliwa Man United mwaka 2019 kwa Pauni 80 milioni akitokea Leicester City.
Akiwa ndio kwanza ana umri wa miaka 21, Josko amekuwa kivutio katika misimu yake miwili na Leipzig tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2021 akitokea Dinamo Zagreb akisifika kwa kutumia nguvu na akili.
“Wakati wote nimekuwa nikiota siku moja nicheze soka England, kufanikiwa kufanya hivyo kwa wakati huu na Manchester City baada ya msimu waliokuwa nao ni heshima kubwa kwangu,” alisema Josko.
Hadi sasa Josko ameichezea timu ya Taifa ya Croatia mara 21 na alitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar ambapo Croatia ilishika nafasi ya tatu.
“Yeyote ambaye aliiona Manchester City ilivyocheza msimu uliopita anajua kuwa ni timu bora duniani, kubeba mataji matatu kunazungumza kila kitu unachotaka kujua kuhusu ubora wa hii timu,” alisema Josko ambaye amekabidhiwa jezi namba 24.
Katika hatua nyingine, Josko alisema kwamba kwake ni furaha kubwa kucheza katika timu moja na mshambuliaji tishio wa Man City, Erling Haaland kuliko wangekuwa timu tofauti.
“Bahati iliyoje niko upande wake kuliko ningekuwa nakabiliana naye, kwa sasa sina haja tena ya kumlinda,” alisema Josko ambaye pia ataungana na nyota mwingine wa Croatia aliyejiunga na timu hiyo, Mateo Kovacic anayecheza nafasi ya kiungo.
Katika misimu yake miwili na Leipzig, Josko alikuwa nguzo imara akisifika kwa kujituma na kutoa mchango mkubwa ulioiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la Ujerumani na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili.
Kimataifa Beki wa nguvu atua Man City
Beki wa nguvu atua Man City
Read also