Na mwandishi wetu
Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kuchezwa kwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na USM Alger, uongozi wa Yanga umesema umepokea tiketi 18,213 kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
Miongoni mwa wadau waliofanikisha kupatikana kwa tiketi za mchezo huo wa kwanza wa fainali hizo, utakaopigwa Jumapili hii, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ni Rais Samia Suluhu Hassan aliyetoa tiketi 5,000.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Benki za NBC, NMB, CRDB na wadau wengine waliochangia na tiketi zimewafikia huku akisema baadhi wametangaza lakini hazijawafikia.
Akizungumza jijini jana Alhamisi, Mkurugenzi wa Matawi na Wanachama Yanga, Haji Mfikirwa alisema mwitikio wa wadau kuchangia tiketi umetokana na hamasa ya Rais Samia tangu atangaze hivi karibuni na wengi wamejitokeza.
“Tangu kuanza utaratibu huu, wanachama wetu na mashabiki wamekuwa wakiuliza utaratibu ukoje wa kugawa tiketi na tunashukuru wadau wote kwa kuchangia kwani hii ni mara ya kwanza kupokea tiketi nyingi kiasi hiki,” alisema.
Alitaja utaratibu wa ugawaji tiketi kwa wanachama na mashabiki kuwa utaangalia wale watakaokuja kwenye mechi uwanjani kutoka matawi yote nchini na kuhimiza makampuni na wadau kuendelea kuunga mkono.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri na kuhimiza watu kuendelea kununua tiketi kwani bado nafasi zipo nyingi.
Alisema wanatarajia kupokea wageni zaidi ya 200 kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na wengine kutoka sehemu mbalimbali kuushuhudia mchezo huo.
Katika hatua nyingine, alisema Ijumaa hii wanatarajia kufanya tamasha la uhamasishaji Mbagala Zakheim litakalohusisha wasanii wote ambao ni mashabiki wa Yanga, vikundi vya hamasa, waigizaji na wachekeshaji.
Pia, alitangaza kuendesha shindano la Twenzetu Algeria ili kupata wanachama na mashabiki watatu watakaosafiri nao katika mechi ya fainali ya pili itakayochezwa Algeria Juni 3, mwaka huu. Washindi wa shindano hilo wanatarajiwa kutangazwa Jumapili hii.
Pamoja na hilo, Yanga wamekabidhiwa vifaa vya ngoma vilivyonunuliwa na wadau kwa lengo ya kuongeza hamasa kwa makundi mawili ya Nyuki wa Kijani na Nyuki wa Njano.