Doha, Qatar
Mshambuliaji mkongwe wa Brazil, Ronaldo de Lima amesema kwamba Neymar na wachezaji wa Brazil wanahitaji kupewa msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na presha kubwa waliyokutana nayo baada ya kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Baada ya Brazil kutolewa na Croatia katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti, Neymar alikiri kwamba jambo hilo ‘lilimvuruga kisaikolojia’.
“Ningeshauri kuwe na msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na presha ambayo kwa hakika ni kubwa mno kwa binadamu,” alisema Ronaldo.
“Neymar baada ya hapo atarudi na hamasa na shauku ile ile, lakini ningependa kusisitiza umuhimu wa kuangalia afya ya akili ya wachezaji wetu, ni muhimu kwetu kulizungumza jambo hilo hasa linapokuja suala la Kombe la Dunia ambapo dunia nzima inaiangalia timu ya taifa, dunia ilikuwa ikimuangalia Neymar,” alisema Ronaldo.
Neymar mwenye umri wa miaka 30 alikuwa na matamanio ya kubeba taji lake la kwanza la dunia akiwa ametoka kupona maumivu wa enka aliyoyapata katika mechi ya kwanza ya Brazil dhidi ya Serbia na kuanza kucheza mechi za hatua ya mtoano.
Tayari alikuwa ameifikia rekodi ya Pele ya kufunga mabao 77 alipofunga bao katika mechi ya robo fainali dhidi ya Croatia lakini bao la kusawazisha la Bruno Petkovic lilizipeleka timu hizo kwenye mikwaju ya penalti ambapo Brazil ilishindwa kutamba.

“Nilipoona kwenye mahojiano Neymar akisema kwamba amevurugwa kisaikolojia, jambo lile liliniumiza moyo katika namna ambayo hata mimi nilivurugwa kisaikolojia, nataka itafutwe namna ya kumsaidia, jambo hilo lipo kwa sasa, katika zama zangu ilikuwa ni nadra jambo hilo kuzungumzwa” alisema Ronaldo.
Ronaldo pia alieleza kushangazwa kwake na wivu na ubaya ambao Neymar alijikuta akikabiliana nao baada ya kuumia katika mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Serbia na kumtaka mchezaji huyo kugeuza wivu na ubaya huo petroli ya kumchochea kufanya vizuri. Baadhi ya mashabiki Brazil walikuwa wakishangilia kuumia kwa Neymar.
