Lverpool, Uingereza
Ndoto za bondia wa Tanzania, Hassan Mwakinyo kutamba katika jiji la Liverpool zilikwama Jumamosi usiku baada ya kuishia raundi ya nne katika pambano la uzito wa super welter dhidi ya Liam Smith.
Raundi ya nne ndiyo iliyokuwa ngumu kwa bondia huyo mwenyeji wa mkoani Tanga ambaye alijikuta akienda chini na hivyo kumfanya mwamuzi Victor Loughlin aanze kumhesabia na wakati Smith akimsogelea Mwakinyo alienda chini tena na kujikuta akisukumiziwa ngumi iliyomfanya aegemee kwenye kamba
Kwa kuona hali inakuwa mbaya kwa Mwakinyo, mwamuzi alionyesha ishara ya kumaliza pambano na hivyo kuzima ndoto ya Mwakinyo kutamba Uingereza kama ilivyokuwa katika pambano lake la awali dhidi ya Sam Eggington.
Kabla ya raundi ya nne, Mwakinyo alionekana kama mtu aliyeumia mguu lakini aliendelea na pambano na kusimama imara huku akimpelekea ngumi mpinzani wake ambazo zilionekana kumpa ujasiri hadi kujikuta akimrushia ngumi wakati kengele ya kumaliza raundi ilishapigwa.
Smith alilianza pambano kwa kuonyesha ubora wake mapema ambapo Mwakinyo wakati akijihami Smith alimrushia ngumi na kuwahi kujikinga na hivyo kumnyima Mwakinyo nafasi ya kujibu shambulizi hilo kwa haraka ingawa alionyesha uimara ambao ni wazi uliwafanya mashabiki kuamini kwamba pambano hilo lingekuwa la muda mrefu kabla mambo hayajaharibika kwenye raundi ya nne.
Baada ya ushindi huo Smith alitamba, “Nimeshangazwa, sijawapa mashabiki ushindi ulio sahihi lakini hilo liko nje ya uwezo wangu, amesema aliteleza, ameshindwa, kwa mshindani makini hawezi kuwa hivyo.”
“Mwanzoni sikuweza kufanya makubwa kwa sababu Hassan alikuwa tishio, nilijua angekuwa hivyo na hatimaye angechoka na mimi ningemmaliza,” alisema na kuongeza kuwa sasa anataka pambano kubwa.
Ushindi huo wa Smith ambao unatambuliwa na mashirikisho ya ngumi ya WBC, WBO na WBA unampa bondia huyo uwezekano wa kupata mapambano mengine makubwa zaidi na kuwa bingwa wa dunia kwa mara nyingine.
Kwa kulifahamu hilo ndio maana Smith alijiandaa vizuri dhidi ya Mwakinyo kwa hofu kwamba huenda kingemkuta kichapo kama kilichomkuta Eggington ambaye ngumi nzito za Mwakinyo zilitosha kumfanya ashuke hadhi yake katika mchezo wa ngumi.
Ngumi Mwakinyo ashindwa kutamba Liverpool
Mwakinyo ashindwa kutamba Liverpool
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
