Berlin, Ujerumani
Uholanzi na England zimefuzu nusu fainali Euro 2024 na sasa zinasubiri kuumana katika mechi ambayo bingwa atacheza mechi ya fainali ya michuano hiyo dhidi ya mshindi wa mechi kati ya Ufaransa na Hispania.
England iliibuka na ushindi wa mabao ya penalti 5-3 Jumamosi hii mbele ya Switzerland baada ya sare ya 1-1 katika dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza wakati Uholanzi imeibugiza Uturuki mabao 2-1.
Switzerland ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za England dakika ya 75 kwa bao la Breel Embolo ambalo lilitosha kuwaweka vichwa chini mashabiki wa England wasiamini kilichotokea.
England ambao katika mechi ya mtoano dhidi ya Slovakia waliokolewa kwa bao la kusawazisha la Jude Bellingham lililosaidia kuwafikisha robo fainali safari hii wameokolewa na bao la Bukayo Saka la dakika ya 80 na kuwapeleka nusu fainali.
Baada ya matokeo hayo, timu hizo zilipambana na kumaliza dakika 90 matokeo yakiwa hivyo hivyo na hata katika dakika 30 za nyongeza hakuna timu iliyopata bao na ndipo sheria ya mikwaju ya penalti ilipotumika na England kutoka na ushindi.
Katika mikwaju ya penalti, England walifunga kupitia Cole Palmer, Jude Bellingham, Saka, Ivan Toney na penalti ya mwisho ya ushindi ilifungwa na Trent Alexander-Arnold.
Aliyewaangusha Switzerland alikuwa ni Manuel Akanji ambaye shuti lake liliokolewa na kipa wa England, Jordan Pickford.
Nao Uholanzi wakiwa nyuma kwa bao 1-0 walifanikiwa kipindua matokeo na kutoka uwanjai na ushindi wa mabao 2-1.

Katika mechi hiyo Uturuki ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 35 lililofungwa kwa kichwa na beki wa kati ya timu hiyo Samet Akaydin akiunganisha krosi ya Arda Guler.
Kipindi chote cha kwanza kilitoa dalili njema kwa Uturuki hasa baada ya kupata bao hilo lakini dakika ya 70 Uholanzi ilisawazisha kupitia kwa Stefan de Vrij aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa.
Dakika saba baadaye mambo yaliwaharibikia, Uturuki baada ya Mert Muldur kujifunga na hivyo kuwazawadia bao la bure Uholanzi.
Mechi za nusu fainali Euro 2024
Jumanne Julai 9, 2024
Ufaransa vs Hispania
Jumatano Julai 10, 2024
England vs Uholanzi
