Abdjan, Ivory Coast
Matokeo mabaya kwenye fainali za Afcon yamesababisha makocha watatu kutoka nchi za Ghana, Algeria na wenyeji wa fainali hizo, Ivory Coast kupoteza kazi hadi sasa.
Kocha wa wenyeji Ivory Coast, Jean-Louis Gasset ametimuliwa baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 4-0 mbele ya Equatorial Guinea, kipigo ambacho kinatajwa kuwa ni kikubwa mno katika historia ya nchi hiyo kwenye Afcon.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Ivory Coast ilieleza kuwa mkataba wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 70 umesitishwa pamoja na ule wa msaidizi wake Ghislain Printant na Emerse Fae amechaguliwa kuwa kocha wa muda.
Kocha mwingine aliyejikuta akipoteza kazi ni Djamel Belmadi wa Algeria ambaye alikubali mwenyewe kusitisha mkataba wake baada ya timu hiyo kutolewa kwenye fainali za Afcon.
Belmadi aliwaambia mapema wachezaji wake kwamba atang’atuka baada ya Algeria kufungwa bao 1-0 na Mauritania.
Rais wa Shirikisho la Soka Algeria, Walid Sadi alisema kwamba alikutana na kocha huyo kwa lengo la kujadili kutolewa kwenye Afcon na mwishowe wakakubaliana kuvunja mkataba wa kocha huyo.
Belmadi alikuwa kocha wa Algeria mwaka 2019 timu hiyo ilipobeba taji la Afcon nchini Misri lakini safari hii timu yake imeishia mkiani na pia ilishindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022.
Chris Hughton (pichani juu) aliyekuwa na kikosi cha Ghana kwenye Afcon naye ametimuliwa baada ya Black Stars kumaliza mechi za Kundi B ikiwa na pointi mbili ikitoka sare mara mbili dhidi ya Msumbiji na Misri na kufungwa mabao 2-1 na Cape Verde.
Ghana ni kati ya timu zilizokuwa zikipewa matarajio makubwa ya kufika mbali lakini juzi Jumanne timu hiyo ilifikia mwisho na kuziaga fainali za Afcon mapema katika hatua ya makundi.
Taarifa ya Chama cha Soka Ghana (GFA) ilieleza kuwa kocha huyo ameondolewa katika majukumu yake pamoja na kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi na siku chache zijazo GFA itatoa mwelekeo wa Black Stars na nini kitakachofanyika.
Kocha Hughton aliingia matatani hivi karibuni baada ya shabiki mmoja kumshambulia kwa maneno lakini GFA wakawa wa kwanza kumtetea kwa kudai kwamba wako pamoja na kocha huyo kwa asilimia 100 lakini hatimaye wameamua kumtimua.
Wakati huo huo hatma ya kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche (pichani) ipo njia panda baada ya kusimamishwa na CAF pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Amrouche amesimamishwa mechi nane kutokana na kauli alizozitoa za kuishutumu Morocco kwa madai ya kuwa na nguvu ya maamuzi ndani ya Caf kuhusu muda wa mechi kuchezwa na uteuzi wa waamuzi.