Manchester, England
Beki Harry Maguire na kipa Andre Onana wa Man United ambao wamekuwa wakilaumiwa kwa uchezaji wa chini ya kiwango, hatimaye wamegeuka mashujaa katika ushindi wa timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Onana na Maguire (pichani juu) walicheza soka la kuvutia wakati Man United ikiibuka na ushindi muhimu wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne hii dhidi ya FC Copenhagen na kuibua matumaini mapya.
Ushindi huo umekuja baada ya kocha wa Man United, Erik Ten Hag kukiri kabla ya mechi kwamba kwa mwenendo wa timu yake suluhisho pekee ni kuhakikisha wanapata ushindi ambao hatimaye ulipatikana huku Onana na Maguire waliopitia kipindi kigumu wakiwajibika ipasavyo.
Maguire alipoteza unahodha Man United huku West Ham ikimtangazia ofa ya kumsajili japo aliikataa ofa hiyo lakini zaidi ya unahodha pia alipoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
Kwa Onana, hivi karibuni baadhi ya mashabiki na wachambuzi walianza kuhoji ni kwa nini hasa Ten Hag alikuwa tayari kutoa kitita cha Pauni 47 milioni ili kumsajili kipa huyo kutoka Inter Milan.
Hata hivyo kuanzia mwishoni mwa wiki wachezaji hao wameanza kuibua matumaini mapya kwa kila mmoja wao kuonesha kile ambacho kimemfanya awe katika klabu hiyo.
Umahiri wa Maguire ulionekana Jumanne si tu katika kudhibiti mashambulizi bali pia ndiye mfungaji bao pekee la ushindi kwa timu yake wakati Onana aliwanyima FC Copenhagen bao la penalti ya Jordan Larsson na hivyo kupata matokeo yaliyofufua matumaini ya timu hiyo kucheza hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
Matokeo mechi za Jumanne Ligi ya Mabingwa Ulaya
Galatasaray 1-3 Bayern Munich
Man United 1-0 FC Copenhagen
Lens 1-1 PSV Eindhoven
Sevilla 1-2 Arsenal
Union Berlin 0-1 Napoli
Sporting Braga 1-2 Real Madrid
Inter Milan 2-1 Red Bull Salzburg
Benfica 0-1 Real Sociedad
Kimataifa Maguire, Onana wageuka mashujaa
Maguire, Onana wageuka mashujaa
Read also