Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ametua nchini kujiunga na timu yake hiyo mpya huku akiahidi kuwapa mashabiki wa klabu hiyo soka la kuvutia.
Gamondi ametua nchini usiku wa kuamkia leo Jumamosi akija kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Nasreddine Nabi aliyeondoka mwisho wa msimu wa 2022-23 baada ya kumaliza mkataba wake.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Gamondi alisema anatumai kuwapa raha mashabiki wa Yanga kwa kuhakikisha timu yake inacheza soka la kuvutia.
“Natumai nitawapa raha (mashabiki) kwa kuhakikisha timu inacheza soka la kuvutia na kushinda mataji,” alisema Kocha huyo raia wa Argentina.
Alisema anafurahi kujiunga na miamba hiyo ya Tanzania akisema sababu ya kuichagua timu hiyo amevutiwa na kile alichoelezwa na Rais wa Yanga, Hersi Said kuhusu mradi wa kukuza vijana na kuwainua.
“Nilitaka changamoto mpya lakini pia nimeelezwa kuhusu mradi ujao nikavutiwa, naamini kwa pamoja tunaweza kutimiza malengo yaliyopo,” alisema Gamondi.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa klabu hiyo Ally Kamwe alisema kutua kwa Gamondi, ni wakati mwafaka kwao sasa kulitangaza rasmi benchi la ufundi jipya kuelekea msimu wa 2023-24.
Alisema pia wanatarajia kuanza harakati za kuwatangaza wachezaji wote wapya waliowasajili kwenye dirisha hili la usajili sambamba na wengine watakaoachwa.
Mpaka sasa Yanga imetangaza usajili wa mchezaji mmoja wa ndani ambaye ni beki wa kushoto, Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate.
