Yaounde, Cameroon
Cameroon imemsimamisha mchezaji aliyeshiriki fainali za Afcon 2023 na timu hiyo kwa kosa la kudanganya jina na tarehe ya kuzaliwa jambo ambalo pia linaweza kuifanya nchi hiyo ifungiwe.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Cameroon (Fecafoot) ilimtaja mchezaji huyo kuwa ni Wilfried Nathan Douala akiwa ni miongoni mwa wachezaji waliosimamishwa katika ligi kwa kwenda kinyume na taratibu ikiwamo majina kugongana na kudanganya umri.
Cameroon ilitolewa katika raundi ya pili ya fainali za Afcon Januari mwaka huu lakini kabla ya hapo kulikuwa na utata kuhusu hatua ya kocha wa timu hiyo, Rigobert Song kumuita Douala katika timu yake.
Douala ambaye ilidaiwa kwamba alikuwa na miaka 17, alikuwa akiichezea klabu ya daraha la pili ya Victoria United na hakuwa na uzoefu wowote kwenye soka la kimataifa.
Mchezaji huyo aliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu wengi walikuwa wakihoji kama kweli alikuwa na miaka 17 mara baada ya picha yake kuonekana hadharani mara ya kwanza.
Uchunguzi wa gazeti la kila siku la Le Monde la Ufaransa ulidai kuwa Douala kabla ya hapo aliwahi kucheza kwenye ligi ya nchini Cameroon kwa jina la Alexandre Bardelli na alikuwa na umri zaidi ya miaka 21.
Siku chache kabla ya timu ya Cameroon kuelekea Ivory Coast kwenye fainali za Afcon, gazeti hilo liliwataka maofisa wanaosimamia soka nchini humo kuelezea utata uliojitokeza kuhusu mchezaji huyo lakini hawakusema lolote.
Mchezaji huyo hata hivyo alibaki kwenye timu ya taifa na kwenda kwenye fainali za Afcon nchini Ivory Coast ingawa hakupata nafasi ya kucheza hata mechi moja.
Kanuni za fainali za Afcon zinasema iwapo kutatokea ukiukwaji wa taratibu au udanganyifu wa aina yoyote, chama cha nchi husika kitasimamishwa kushiriki fainali hizo kwa michuano miwili inayofuata.
Afcon2024 Mchezaji Cameroon adaiwa kudanganya umri, jina
Mchezaji Cameroon adaiwa kudanganya umri, jina
Related posts
Read also