Kim: Tupo tayari kusaka ushindi
Na mwandishi wetu
Timu ya Taifa, Taifa Stars leo majira ya saa moja usiku inatarajia kucheza mechi yake ya kwanza ya kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2023 kwa kukipiga na Niger huku kocha wa Stars, Kim Poulsen akieleza kuwa vijana wako tayari kupambania ushindi katika mchezo huo.
Kim amesema pamoja na kukiandaa vyema kikosi chake lakini pia wamewatazama wapinzani wao kwa njia ya video na kuona ilipo nguvu yao na idhaifu wao kwa ajili ya kuhakikisha wanafanikiwa kupata matokeo kwenye mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa L’amitie jijini Cotonou, Benin.
Imeelezwa kuwa Niger imeipeleka mechi hiyo Benin kutokana na viwanja vya kwao kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
“Tumemaliza mazoezi yetu ya mwisho na wachezaji wanaonekana wako tayari kwa ajili ya mechi na kuanza safari yetu ya kucheza Afcon, ni michuano inayoanza upya kwa hiyo na sisi tunajua tunataka nini ndiyo maana tunaiangalia zaidi mechi hii ya kwanza.
“Kwenye mpira tunasafiri na kufanya mazoezi, kujifunza kila siku ni kwa ajili ya kuonesha mchezo mkubwa na tunafahamu uzuri wa Niger, tumeona video zao, wana washambuliaji wazuri na wakakamavu ambao tutahitaji kuwadhibiti huku nasi tukitafuta namna ya kuwafunga, tunakwenda kupambana na vijana wako tayari kwa mechi,” alisema Kim.
Naye wa mshambuliaji wa timu hiyo, Simon Msuva alisema: “Sisi kama wachezaji tuko tayari kwa ajili ya mchezo huu naamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutashinda na tunauhitaji mchezo huu hata ukiangalia maandalizi yamekuwa mazuri na mwalimu mwenyewe, sisi pia tumewaona wapinzani wetu, naamini tupo tayari kupambana katika mechi hii.”
Stars iliyo Kundi F inawania kushiriki michuano hiyo nchini Ivory Coast, inayotarajia kufanyika Juni 23 mpaka Julai 23, mwakani dhidi ya timu za Niger, Algeria na Uganda.
