Yaounde, Cameroon
Hali bado tete katika soka Cameroon baada ya shirikisho la soka nchini humo, Facefoot ambalo linaongozwa na mwanasoka wa zamani, Samuel Eto’o kumuweka kando kocha mkuu, Marc Brys (pchani) .
Uongozi wa Facefoot umekuja na azimio hilo baada ya kuibuka mzozo kati ya kocha huyo na Eto’o na tayari shirikisho hilo limemteua Martin Ndtoungou kuwa kocha wa muda wa timu hiyo.
Brys, kocha kutoka Ubelgiji ambaye aliteuliwa na serikali, juzi Jumanne alizozana na Eto’o na sasa hatokuwa na timu hiyo inayojiandaa kwa mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Habari za ndani zinadai kwamba viongozi Facefoot hawakukubaliana na uteuzi wa kocha huyo ambao ulifanywa Aprili mwaka huu na serikali kupitia wizara ya michezo bila ya kuwashirkisha viongozi wa shirikisho hilo.
Katika mzozo wa Jumanne, Brys alialikwa katika ofisi za Facefoot kwenye kikao cha kupanga mikakati ya kazi lakini baadhi ya wasaidizi wake walizuiwa kuingia kwenye jengo la ofisi za shirikisho hilo mjini Yaounde.
Baada ya tafrani hiyo, Eto’o na kamati yake katika Facefoot wakaitisha kikao cha dharura na ndicho kilichofikia uamuzi wa kumuweka kando Brys jambo ambalo ni wazi litaliingiza shirikisho hilo katika mgogoro na serikali.
Timu ya Cameroon au Indomitable Lions, katika mbio za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, hadi sasa ina pointi nne baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare moja, Juni 8 itaumana na Cape Verde kabla ya kucheza na Angola siku tatu baadaye.
Kimataifa Eto’o amuweka kando kocha mkuu Cameroon
Eto’o amuweka kando kocha mkuu Cameroon
Read also
