Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa FC Lupopo, George Mpole ameeleza kuwa anafikiria juu ya ofa alizonazo za kuhamia timu nyingine kutokana na hali isiyoridhisha ya Ligi Kuu DR Congo kwa sasa.
Mpole ameiambia GreenSports leo Alhamisi kuhusu kufutwa kwa ligi hiyo msimu huu maarufu Ligi 1 huku akiwa hajacheza hata mechi moja tangu atue kwenye kikosi hicho msimu huu akitokea Geita Gold.
Alifafanua kuwa kinachoendelea sasa hakina afya kwenye maendeleo yake ya soka hivyo atakaporejea nyumbani Tanzania ataangalia cha kufanya ili kuepukana na hali iliyomtokea kwa sasa.
“Ligi imefutwa mpaka msimu ujao, mimi si mwenyeji huku siwezi kufahamu sana mambo yao lakini kinachotokea si kizuri kwa maendeleo yangu ya soka kwa namna navyohitaji kufika mbali hivyo lazima nijue nafanyaje,” alisema Mpole.
“Nikifika huko (Tanzania), nitakuwa karibu zaidi na washauri na wasimamizi wangu tutaangalia cha kufanya, namna ya kukabiliana na hilo maana ofa zipo za nchi za nje na hata Tanzania, hivyo tutajua cha kufanya,” aliongeza Mpole.
Mchezaji huyo aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita kwa mabao 17 amesema kuwa kwa sasa anasubiri tarehe na mipango ya safari kutoka kwa mabosi wake wa Lupopo na wiki ijayo anatarajia kuwa amerejea nchini kusubiri ratiba mpya ya ligi hiyo msimu ujao.
Mpole aliyesaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo hakufanikiwa kuitumikia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwani tayari alishacheza michuano hiyo akiwa na Geita.
“Sikucheza kwenye Kombe la Shirikisho na kwenye ligi pia hakukuwahi kuwa na mechi hadi tulipokuja kuambiwa ligi imesimama kisha imefutwa, hivyo tulikuwa tunacheza mechi nyingi za kirafiki tu,” alisema Mpole.