London, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema bado ana matumaini ya timu hiyo katika mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu wa 2025-26 licha ya timu yake kuachwa na vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi sita.
Mbio za Man City katika taji hilo msimu huu ziliingia doa Jumapili ya Januari Mosi, 2026 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Tottenham na kuwafanya baadhi ya mashabiki kuanza kupoteza matumaini na timu hiyo.
Katika mechi hiyo Man City ilionekana kuwa vizuri na hadi mapumziko timu hiyo ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 lakini baadaye waliruhusu mabao mawili na kufanya mechi iishe kwa sare ya 2-2.
Pep hata hivyo haamini kama matokeo hayo yanatosha kuitoa timu yake katika mbio za kulisaka taji hilo badala yake anaamini timu yake bado ina nafasi katika mbio hizo.
“Inapotokea kuna nafasi na matumaini wakati wote yanakuwapo, nazijua mechi za aina hii wakati wote kuna namna ya kushinda lakini leo (Jumapili) haikuwa hivyo,” alisema Pep.
Pep pia alisema kwamba timu yake imekuwa ikikutana na mambo mengi magumu lakini wachezaji wake wamekuwa wakikabiliana nayo na amekuwa akishuhudia upambanaji katika namna nzuri kwenye mambo mengi.
Kocha huyo pia katika wiki chache zilizopita amekuwa akilalamikia waamuzi na katika mechi yake na Tottenham alisema kuna baadhi ya mambo hayakumfurahisha ikiwamo bao la kwanza la Tottenham.
