Cotonou, Benin
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo imetoka sare ya bao 1-1 katika mechi yake ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) iliyopigwa kwenye dimba la L’amitie jijini Cotonou, Benin.
Stars ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya kwanza ya mchezo huo lililofungwa na mpachika mabao wa Geita Gold, George Mpole aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa baada ya kipa wa Niger kulitema shuti la Simon Msuva na Mpole kuuwahi mpira huo.
Iliwachukua dakika 24 Niger kusawazisha bao hilo wakineemeka na bao la Daniel Sosah ambaye akiwa karibu kabisa na lango la Stars aliuwahi mpira uliotokana na pasi ndefu na kuwazidi ujanja mabeki wa Stars.
Hadi timu zinakwenda mapumziko ni Niger ndio walioonyesha uhai kwa kuliandama lango la Stars lakini juhudi zao hazikuzaa matunda licha ya kuongoza katika kuumiliki mpira wakiwa na asilimia 51.3 dhidi ya 48.7 za Stars.
Kipindi cha pili, Stars nao walionekana kuwa na uhai, washambulaiji wake Mbwana Samatta alikosa bao la kichwa baada ya mpira alioupiga kutoka nje sentimita chache wakati Kibu Dennis aliyeingia kuchukua nafasi ya Mpole naye aliuwahi mpira upande wa kulia baada ya kumzidi kipa wa Niger aliyetoka lakini shuti la chinichini la Kibu liligonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Niger.
Kwa matokeo hayo timu hizo za Kundi F zimegawana pointi huku zikisubiri matokeo ya mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Algeria na Uganda ambayo pia inachezwa baadaye usiku huu. Stars itajitupa tena uwanjani Juni 8 dhidi ya Algeria, mechi inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam
